1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Miezi miwili ya shambulio la Palma, manusura bado wanakimbia

24 Mei 2021

Miezi miwili tangu mashambulizi ya wapiganaji wa itkadi kali za Kiislamu dhidi ya mji wa Palma jimboni Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji, manusura wa mashambulizi hayo bado wanaendelea kukimbia kuokoa maisha yao.

Mosambik Palma | nach Angriff von Rebellen
Picha: Dave LePoidevin/MAF/AP/picture alliance

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM, vurugu za hivi karibuni katika wilaya ya Palma nchini Msumbiji zimesababisha kupoteza makazi kwa watu takriban elfu 57 katika muda wa wiki nane zilizopita.

Serikali inasema kuwa mamia ya watu waliuawa katika mwezi wa Machi na siku chache baadaye kusema kuwa imechukuwa udhibiti wa eneo hilo na hakuna vyombo vya habari ambavyo vimeruhusiwa mjini humo tangu ziara mbili za kijeshi zilizopangwa mnamo Machi.

Watu wengi hawajui pa kuanzia huku Fransisco akiwa na afueni kwamba sasa yuko salama mjini Pemba ambao ndio mji mkuu wa mkoa wa Kaskazini wa Cabo Delgado.

Soma piaWakuu wa SADC walaani uasi nchini Msumbiji

Fransisco wa umri wa miaka 21 ambaye sasa ni mama wa mtoto wa siku nne, alitumia siku nane ndani ya boti na nyingine tatu katika ufuo wa bahari kabla ya kuhamishwa na kupelekwa katika kituo cha muda katika uwanja mmoja wa michezo.

Watu wengi waliotoroka mashambulizi ya wapiganaji mjini Palma, wamo katika kituo cha mpito cha watu waliokosa makaazi mjini Pemba, mji mkuu wa jimbo la Cabo Delgado.Picha: DW

Akiwa na ujauzito wa miezi saba, Franscisco alikuwa nyumbani wakati wanamgambo wa kundi la al-Shaabab walipolivamia eneo hilo la Palma ambalo wakazi huamini kuwa ni salama lisiloweza kuvamiwa kutokana na mamia ya wanajeshi wanaolinda mradi wa gesi wa thamani ya mabilioni ya dola.

Kilichofuatia uvamizi huo wa Machi 24 ni mfululizo wa machafuko. Wakati milio ya risasi ilipoanza kusikika alasiri hiyo, watu hawakutarajia kuwa huenda likawa ni kundi la al-Shaabab jina linalotumika katika eneo hilo kumaanisha wanamgambo.

Wakati walipotambua kinachoendelea, wanamgambo hao tayari walikuwa wameanza kuzingira vijiji vyote mjini humo na watu kuanza kutoroka. Franscisco ameliambia shirika la habari la AFP kwamba alifahamu kuwa iwapo asingekimbia, angekamatwa.

Soma pia: Mapigano kaskazini mwa Msumbiji yaendelea

Siku kadhaa zilizofuata, mamia ya watu walihamishwa kwa ndege na mashirika ya msaada wa kiutu ama na usafiri wa kampuni za kibinafsi lakini wengi waliachwa kujishughulikia wenyewe katika mji wa Quitunda ulioko karibu na kiwanda cha gesi kilicho chini ya ulinzi mkali.

Watu wanaokimbia mapigano wakiwasili baada ya kuondolewa na ndege katika mji mkuu wa jimbo la Cabo Delgado wa Pemba, Aprili 21, 2021.Picha: Dave LePoidevin/MAF/AP/picture alliance

Kila moja anataka kuondoka Palma

Juhudi za kuwaondoa wakimbizi hao mjini Quitunda bado zinaendelezwa. Maboti ya uvuvi ya kibinafsi yanatoza kiasi cha dola kati ya 50 na 80 kwa safari hadi Pemba, hiki kikiwa kiwango cha juu kwa eneo hilo maskini.

Wakimbizi wanaowasili mjini Pemba wanazungumzia kuhusu watu wengi wanaotaka kuondoka Quitunda. Mashirika ya msaada yanakadiria kuweko kwa takriban watu elfu 20 katika eneo hilo. Karibu kila siku, maboti madogo yaliyobeba watu huwasili mjini Pemba kutoka wilaya ya Palma.

Soma pia: Raia wateseka na mauaji, utekaji kaskazini mwa Msumbuji

Mwishoni mwa wiki, rais Filipe Nyusi, alisema kuwa siku ya Ijumaa, wanamgambo hao walijaribu kuvamia mji wa Olumbe wilayani Palma bila mafanikio. Ghadhabu inayotaka na kushindwa kwa serikali kushughulikia tatizo hilo inaongezeka.

Daniel Chilongo, mkulima wa umri wa miaka 55 katika eneo hilo, anasema kuwa wakati uvamizi huo ulipoanza, wanamgambo walikuwa wanatumia mapanga lakini serikali haikuchukuwa hatua yoyote kukabiliana nao na kwamba kufikia sasa, wanamgambo hao wamegeuza mtindo na kuanza kutumia silaha za kisasa.

Viongozi wa kanda ya Kusini mwa Afrika, wanatarajiwa kukutana baadaye wiki hii kuzungumzia kuhusu njia za kushughulikia ghasia hizo huku kukiwa na uvumi watashinikiza kupelekwa kwa wanajeshi 3,000.

Chanzo: AFP

    

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW