1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Migawanyiko ya kisiasa Sudan Kusini imezidisha uhasama

Sylvia Mwehozi
27 Aprili 2021

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa migawanyiko ya kisiasa na kikabila huko Sudan Kusini imeongezeka na kusababisha matukio ya vurugu baina ya pande zilizosaini usitishaji mapigano na pia uwezekano wa kuzuka upya vita.

Südsudan Salva Kiir und Riek Machar | Entscheidigung für  Einheitsregierung
Picha: Reuters/J. Solomun

Ripoti ya kurasa 81 iliyotolewa Jumatatu inasema kasi ndogo ya mageuzi katika serikali ya Rais Salva Kiir na mvutano wa kisiasa uliodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja na tofauti za utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano ya Februari mwaka 2020 pamoja na makubaliano ya amani ya mwaka 2018, vimechochea uhusiano hafifu baina ya Kiir na makamu wake wa rais Riek Machar.

Jopo hilo la wataalam limesema kumekuwa na hali ya kutoridhika ndani ya chama cha rais Kiir cha Sudan People's Liberation Movement SPLM na mamlaka yake ndani ya kabila la Dinka, juu ya namna alivyoshughulikia kipindi cha mpito na kuchochea wito wa uongozi mpya. Ripoti hiyo imenukuu vyanzo kadhaa katika kambi ya Kiir vikisema kumekuwa na migawanyiko juu ya mgawanyo wa nafasi za serikali. Jitihada za rais Kiir za kushughulikia mivutano ya ndani miongoni mwa wafuasi wake zimeshindwa na kusababisha matukio ya kiusalama nje ya mji mkuu.

Kwa upande wa Machar, jopo hilo linadai kuwa kushindwa kwake kuwa na ushawishi katika maamuzi ya serikali au kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano kumechangia jeshi la SPLM ndani ya upinzani, ambao unaongozwa na Machar kuanza kugawanyika. Baadhi ya viongozi wa kisiasa na kijeshi ndani ya kambi ya Machar wameanza kupinga uongozi wake na wengine kukimbilia upande wa serikali.

Wanajeshi wa Sudan Kusini katika mapambano mwaka 2016Picha: picture-alliance/Photoshot/Xinhua/G. Julius

Kulikuwa na matumaini makubwa ya amani na utulivu wakati taifa hilo lenye utajiri wa mafuta lilipojipatia uhuru wake kutoka Sudan. Lakini nchi hiyo ilitumbukia katika machafuko ya kikabila mwaka 2013 wakati vikosi tiifu kwa Rais Kiir vilipoanza kupambana na vile vya hasimu wake Machar anayetoka kabila la Nuer.

Sudan Kusini yasaini mkataba wa amani na wanamgamboJitihada kadhaa za kurejesha amani zimegonga ukuta ikiwa ni pamoja na mkataba ambao ulimrejesha Machar katika nafasi ya umakamu wa rais mwaka 2016 na kisha kukimbia miezi michache baadae katikati mwa mapigano mapya. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vimewauwa karibu watu 400,000 na mamilioni kukosa makaazi.

Kulingana na ripoti hiyo vikosi vya usalama vya serikali hivi sasa vinadhibiti rasilimali nyingi za umma kwa kuanzisha makampuni huru ya ukusanyaji mapato. Wataalamu hao wanaonya kwamba kushindwa kufikia utekelezaji wa masuala muhimu katika serikali ya umoja wa kitaifa unafanya "utulivu wa Sudan Kusini kubaki katika hatari". Nyongeza ya hayo ni kwamba nusu ya idadi ya wakaazi wa taifa hilo wanakabiliwa na "kitisho kikubwa cha usalama wa chakula" na karibu watu laki moja kwenye maeneo kadhaa wamo katika hali inayokaribiana na baa la njaa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW