1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Migogoro na uhaba wa chakula

29 Januari 2019

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inaonyesha uhusiano uliopo kati ya migogoro na uhaba wa chakula. Ripoti hiyo inasema mamilioni ya watu katika maeneo ya mizozo wanahitaji msaada wa dharura. 

Südsudan WFP Schüler
Picha: WFP

Ripoti hiyo inasema viwango vya utapiamlo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Sudan Kusini, Yemen na Afghanistan vilizorota kabisa mwishoni mwa mwaka wa 2018.

Kwa upande mwingine, hatua zimeonekana kupigwa kiasi katika nchi za Somalia, Syria na eneo la Ziwa Chad, na hii, kwa mujibu wa ripoti hiyo, inatokana na hali iliyoimarika ya usalama.

Kwa jumla, karibu watu milioni 56 katika maeneo manane ya mizozo wanahitaji msaada wa dharura wa chakula na kuwasaidia kimaisha, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa. Lile la Chakula na Kilimo – FAO na la Mpango wa Chakula Duniani – WFP.

Utafiti huo "unadhihirisha wazi athari za migogoro ya kivita kwa maisha ya mamilioni ya wanaume, wanawake, wavulana na wasichana wanaojikuta katika migogoro hiyo.

Mmoja ya watu waliokimbia makazi yao Nigeria akiwa amebeba chakula cha msaada. Raia hawa wamekimbia mashambulizi ya wanamgambo wa Boko Haram.Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Mkurugenzi Mkuu wa FAO Jose Graziano da Silva anaeleza kuwa watu wanapaswa kufahamu kwamba nyuma ya takwimu hizo zinazotolewa na mashirika hayo ya kimataifa, kuna watu wanaokabiliwa na viwango vya kutisha vya njaa ambavyo havikubaliki kamwe katika karne ya 21.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa WFP David Beasley anasema Umoja wa Mataifa unahitaji kuingia kwa njia bora na ya haraka sana katika maeneo ya mizozo ili kutoa msaada. Lakini ameongeza kuwa kile ulimwengu unahitaji Zaidi ya yote ni kusitishwa kwa vita vonavyoendelea kushuhudiwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vitendo vya machafuko dhidi ya wafanyakazi wa kiutu vimeongezeka, ambapo mara nyingine husababisha kusitishwa kwa operesheni za mashirika hayo na hivyo kuwanyima msaada watu walioko hatarini.

Kupungua kabisa kwa hifadhi ya chakula kunatarajiwa mwaka huu katika msimu wa kuanzia Juni hadi Agosti katika kanda ya Ziwa Chad, yakiwemo maeneo ya Nigeria na Niger, ambako wanamgambo wa Boko Haram wanaendesha harakati zao.

Mwandishi: Bruce Amani(AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga