1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Migogoro yaendelea kuligubuika bara la Afrika

Mohammed Abdulrahman3 Mei 2005
Wapinzani wakiandamana katika mji mkuu wa Togo-Lome.
Wapinzani wakiandamana katika mji mkuu wa Togo-Lome.Picha: AP

Bara la Afrika bado limeandamwa na migogoro kuanzia Ivory Coast na Togo katika Afrika magharibi hadi Somalia, mashariki mwa bara hilo. Kuhusu Ivory Coast, ripoti ya Shirika linalotetea haki za binaadamu Human Rights Watch, inasema kwamba nchi hiyo inakabiliwa na hatari ya kuingia katika umwagaji damu zaidi na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu.

Tukianzia na Ivory coast, kwa mujibu wa Shirika hilo la Human Rights Watch, kusambazwa kwa wanamgambo wasio na mafunzo ya kutosha wala nidhamu, huenda kukazidisha vitendo vya kuwabughudhi raia . Kwa mujibu wa ripoti ya kurasa 35 hali ya wasi wasi wa kikabila, magharibi mwa taifa hilo kuu la kilimo cha kokoa duniani, na ambapo watu kiasi ya 14 waliuwawa katika mapigano baina ya wahamiaji na wakulima wa eneo hilo karibu na mji wa Duekoue, yanazusha kitisho cha hali kuweza kuwa mbaya zaidi.

Imesema jumuiya za kanda hiyo, serikali za eneo hilo na pia mahakama ya uhalifu ya kimataifa, hazina budi kufuatilia na kuhakikisha wanaohusika katika kuchochea mgogoro huo nchini Ivory Coast wanawajibika mbele ya vyombo vya kisheria.

Ivory Coast imeingia katika mgogoro kati ya waasi upande wa kaskazini na serikali inayoungwa mkono na wanamgambo upande wa kusini tangu uliposhindwa uasi wa Septemba 2002 na kuzusha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Matumaini ya kupatikana suluhisho yamekua yakizuka na kufifia wakati mmoja, licha ya makubaliano ya amani ya karibuni yaliosainiwa baada ya mazungumzo ya pande zinazohusika katika mji wa Afrika kusini wa Pretoria chini ya Uapatanishi wa rais Thabo Mbeki wa nchi hiyo, kwa niaba ya Umoja wa Afrika.

Wadadisi wanasema Kuendelea kwa mgogoro wa Ivory Coast, kunaweza pia kuuhujumu utaratibu wa amani unaolega lega katika nchi jirani ya Liberia na hata kuchangangi katika kuzusha hali ya msuko suko katika nchi jirani ya Guinea.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Shirika la Human Rights Watch katika Afrika Peter Takirambudde anasema kuna matumaini kwamba mkataba wa amani wa hivi karibuni ambao ni pamoja na hatua ya kusalimisha silaha na kufanyika uchaguzi Oktoba 30 mwezi huu, unatarajiwa kuboresha hali ya ukiukwaji wa haki za binaadamu nchini Ivory Coast.

Wasi wasi mwengine katika eneo hilo, ni nchini Togo, kufuatia matokeo ya uchaguzi wa rais wa Aprili 24 ambapo mshindi alitangazwa kuwa mgombea wa chama tawala Faure Eyadema , mtoto wa Rais wa zamani wa chini hiyo Gnassingbe Eyadema aliyefariki dunia mwezi Februari baada ya kuitawala Togo kwa miaka 37. Mgombea wa upinzani Emmanuel Bob Akitani aliyepata 38 asili mia ya kura kwa mujibu wa tume ya uchaguzi dhidi ya 60 asili mia za mpinzani wake. Akajitangaza Urais, lakini wachunguzi kutoka Jumuiya ya kichumi ya Afrika magharibi ECOWAS wakaidhinisha matokeo.

Maelfu ya wakaazi wamekimbilia nchini jirani za Benin na Ghana kujinusuru na machafuko. Hadi jana hata hivyo mji mkuu Lome ulikua shwari. Wakati vuta nikuvute ikierndelea Faure Eyadema ameutaka upinzani ushiriki katika serikali itakayoundwa ya umoja wa taifa. Ama Bw Akitani Bob alipinga pendekezo hilo, huku mpinzani mwengine harry Olimpio akisema serikali yoyote ya upatanishi wa taifa haina budi isimamiwe na Jumuiya ya kimataifa.

Mbali na matatizo hayo ya kisiasa katika nchi hizo mbili za Afrika magharibi, Somalia nayo inaendelea kuugubika umoja wa Afrika, huku serikali ya mpito ikiwa bado Nairobi-Kenya na kushindwa kurudi nyumbani kwa sababu ya hali mbaya ya usalama. Sambamba na hayo maachafuko yameendelea nyumbani huku jana kiasi ya watu 8 wakiuwawa na 28 kujeruhiwa katika mripuko kwenye uwanja wa michezo mjini Mogadishu, ambako Waziri mkuu wa mpito Ali ohamed Gedi alikua akiuhutubia umati mkubwa wa watu. Hapo kabla Bw Gedi aliwataka wababe wa kivita kusalimisha silaha zao ili serikali ya mpito iweze kurudi nyumbani.

Umoja wa Afrika unatazamiwa kuanza karibuni zoezi la kutumwa wanajeshi wapatao 10,000 wa kulinda amani kutoka nchi za jumuiya ya mataifa jirani ya IGAD. Lakini hadi pale amani itakaporejea katika nchi hiyo iliingia katika vita vya wenyewe kwa wenbye tangu 1991 baaada ya kuangusha dikteta Mohamed Siad Barre, Somalia sawa na migogoro mengine kama Ivory Coast na Togo inaendelea kuugubika umoja wa Afrika-AU.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW