1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Migomo yahanikiza Ugiriki na Hispania

Oumilkher Hamidou29 Juni 2010

Wafanyakazi wa Ugiriki na Hispania wateremka majiani kupinga hatua za kufunga mikaja

Maaandamano mbele ya bunge la Ugiriki mjini AthensPicha: AP

Migomo na maandamano yamezigubika Ugiriki na Hispania hii leo na kutoa sura jumla ya upinzani wa wakaazi wa Ulaya dhidi ya hatua za kufunga mikaja.

Nchini Ugiriki polisi wa kuzuwia fujo wametumia gesi za kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokua wakipaza sauti kutaka bunge lichomwe moto hii leo mjini Athens, muda mfupi kabla ya wabunge kujadiliana juu ya mswaada wa mageuzi ya malipo ya uzeeni-hatua inayopingwa na wengi wa wakaazi wa Ugiriki. Zaidi ya watu elfu kumi wameteremkia majiani mjini Athens wakishiriki katika mgomo watano mkubwa kuitishwa mwaka huu nchini humo ili kupinga hatua za kufunga mikaja zilizoamuliwa na serikali.

Mgomo huo ulioitishwa na vyama vya wafanayakazi wa sekta ya kibinafsi na ya serikali umeathiri shughuli za utawala, sekta ya elimu, benki na vyombo vya habari pia.

"Tieni moto bunge-ndio kauli mbiu ya vijana kama 150 hivi waliofunika nyuso zao, huku wakivurumisha magongo, mawe na mabomu ya mikono dhidi ya polisi waliokua wakilinda majengo ya serikali mjini Athens.

"Tumerejea tena majiani, tunagoma kwa sababu hatutaki haki zetu zikanyagwe", amesema hayo Ilias Vrettakos ambae ni naibu mwenyekiti wa chama kikuu cha wafanya kazi wa serikali.

Bandari imezingirwa huko Piree, safari za ndege zimezuwiliwa kutoka Athens hadi visiwa vingine vya Ugiriki, hata hivyo, safari za kimataifa zimeendelea. Migomo na maandamano imeathiri pia sekta ya utalii nchini Ugiriki-sekta inayowakilisha asili mia 20 ya pato la ndani la Ugiriki.

Mswaada kuhusu mageuzi ya mfumo wa malipo ya uzeeni utajadiliwa bungeni kuanzia July nane ijayo na unataka waatu wafanye kazi kwa muda wa miaka 40 badala ya miaka 37, kabla ya kustaafu na kufutilia mbali mitindo ya watu kustaafu kabla ya wakati nchini Ugiriki.

Bango lililoandikwa"mizogo wabebe benki"Picha: AP

Nchini Hispania pia wananchi wameteremka majiani mjini Madrid hii leo kulalamika dhidi ya hatuia za kufunga mikaja. Njia za usafiri wa chini kwa chini mjini Madrid zinazotumiwa na zaidi ya watu milioni mbili wa jiji hilo zimefungwa na kuwalazimisha wenyeji na wageni watafute njia nyengine za usafiri kwenda kazini au uwanja wa ndege.

Mgomo huo ambao si kawaida kutokea katika hali kama hiyo umeitishwa na vyama vya wafanya kazi kulalamika dhidi ya mipango ya kupunguzwa mishahara kwa asili mia tano watumishi wote wa serikali wa eneo hilo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Madrid, hii ni mara ya kwanza tangu miaka 20 iliyopita kwa mgomo kama huo kuvuruga shughuli za usafiri mjini Madrid.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Afp,Reuters

Imepitiwa na : Miraji Othman