1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Miili 60 yapatikana baada ya operesheni ya Israel

12 Julai 2024

Maafisa katika eneo linalodhitiwa na Hamas wamesema takriban miili 60 imepatikana kwenye vifusi katika viunga vya mji wa Gaza. Hii baada ya jeshi la Israel kutangaza kusitisha operesheni yake katika eneo hilo.

Gaza | Uharibifu baada ya shambulio la Israeli
Mtazamo jumla unaonyesha eneo la mashambulizi ya Israel kwenye makaazi.Picha: Ayman Al Hassi/REUTERS

Hii baada ya jeshi la Israel kutangaza kusitisha operesheni yake katika eneo hilo. Huku haya yakijiri rais wa Marekani Joe Biden amesema mazungumzo juu ya mpango unaowezekana wa kusitisha mapigano "yanapiga hatua."

Soma pia: Hamas yasema haijapokea taarifa kutoka kwa wapatanishi

Israel imevurumisha makombora katika mji wa Gaza kwa wiki moja mfulizo, hatua ambayo wakazi wameitaja kama vita vikali zaidi tangu mashambulizi yalipoanza. Israeli imekuwa ikiishambulia Gaza kwa muda wa miezi 10 katika vita ambavyo vimeharibu maeneo na kuua zaidi ya Wapalestina 38,000, kulingana na mamlaka za afya huko Gaza.

Miili hiyo 60 imepatika baada ya wanajeshi wa Israel kumaliza operesheni ya wiki mbili ambayo Jeshi la Ulinzi la Raia la Gaza na wakaazi wanasema imeacha eneo hilo kuwa magofu. Msemaji wa Ulinzi wa Raia Mahmud Bassal amesema asilimia 85 ya majengo yameharibiwa na kulitaja eneo la Shujaiya kama "eneo la maafa".

Magari ya jeshi la Israel katika mji wa Rafah wakati wa operesheni dhidi ya kundi la Hamas.Picha: Ohad Zwigenberg/dpa/AP/picture alliance

Kwa mujibu wa mamlaka ya Palestina, takriban watu sita waliuwawa Alhamisi katika mashambulizi ya anga ya Israel katika jiji la Gaza na wengine 19 katika maeneo mengine ya Ukanda wa Gaza. Huduma ya dharura ya raia imeripoti kwamba miili ya Wapalestina wasiopungua 30 waliouawa imetawanyika kwenye barabara zisizoweza kufikiwa katika Jiji la Gaza.

Mapigano yalipamba moto kutoka kaskazini hadi kusini mwa eneo la pwani huku mazungumzo yakiendelea kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka.

Israel yalenga miundo mbinu

Jeshi la Israel limesema wanajeshi wanaendelea na operesheni mjini Rafah, karibu na mpaka wa Misri. Katika taarifa yake  limedai pia kuwauwa wanamgambo wengi katika mapambano ya ardhini na mashambulizi ya anga, na kwamba wameharibu miundombinu ya ugaidi katika eneo hilo.

Israel yazidisha mashambulizi katika ukanda wa Gaza

01:35

This browser does not support the video element.

Huku haya yakijiri rais wa Marekani Joe Biden amesema mpango wake wa kusitisha mapigano Gaza umekubaliwa na Israel na kundi la Hamas. Hata hivyo Biden amekiri  kuwa bado kuna "mapengo ya kuziba".

"Wiki sita zilizopita, niliweka mpango wa kina kwa maandishi. Uliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na kundi la G7. Mfumo huo sasa unakubaliwa na Israel na Hamas. Haya ni masuala magumu na yenye changamoto. Bado kuna mapungufu. Kuna maendeleo. Mwenendo ni mzuri, na nimeazimia kukamilisha mpango huu na kukomesha vita hivi, ambavyo vinapaswa kumalizika sasa. "Soma pia: Netanyahu kupeleka wawakilishi majadiliano ya kusitisha vita Gaza

Mazungumzo hayo ambayo Marekani, Misri na Qatar yanapatanisha yanalenga juu ya mpango wa hatua tatu uliowekwa na Biden mnamo Mei. Mpango huo unalenga kubadilishana mateka wa Israel kwa wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa Jela za Israel pamoja na kuanzishwa kwa usitishaji mapigano wa kudumu katika mzozo wa Gaza.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW