Miito ya kuachiwa wafungwa wa kisiasa Sudan Kusini yatolewa
11 Januari 2014Hapo jana katibu mkuu huyo alisema, amezungumza na rais Salva Kiir Alhamis na kutoa wito wa kuachiwa huru maafisa wa upinzani kwa lengo la kuongeza matumaini ya kumaliza vita ambavyo inahofiwa maelfu wamekufa tangu Desemba 15. Ban ameyasema hayo wakati alipozungumza na waandishi wa habari mjini New york. Katibu Mkuu amenukuliwa akisema "Nimempigia rais Salva Kiir jana kwa mara nyingine na nimemtaka afanikishe uongozi wake kwa vitendo na kisiasa kwa kuwaachia huru mara moja wafungwa wa kisiasa". alisema Ban.
Baraza la Usalama larejea wito wa kusitishwa mapigano
Mataifa 15 wanachama wa baraza la Usalama vilevile yametaka kuachiwa huru kwa wanasiasa hao kwa lengo la kufanikisha mazingira bora ya mazungumzo yenye tija kati ya Kiir na makamo wa rais wa zamani Riek Machar. Wanadiplomasia wanasema Machar anataka kuachiwa huru kwa wanasiasa 11 waandamizi kabla ya hatua yoyote ya kusitisha mapigano, ambao vilevile Kiir anasisitiza lazima wakabiliane na mkono wa sheria. Majeshi tiifu kwa Kiir na Machar yanaendelea kupambana kuwania miji muhimu wakati mazungumzo ya amani yakiendelea mjini Adis Ababa, Ethiopia.
Taarifa za mataifa hayo 15 imezitaka pande zote zinazohasimiana kuacha mapigano mara moja bila kuwepo kwa masharti yoyote. Katibu Mkuu Ban Ki-moon anasema hali ya Sudan Kusini imefikia katika hatua mbaya sana ambao inakadiriwakiasi ya watu 75,000 kutoka katika maeneo tofauti ya taifa hilo wamekusanyika katika eneo la ofisi za Umoja wa Mataifa.
Vitendo vya ukiukwaji wa haki za binaadamu vyabainika
Aidha,kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amesema vitendo vya ukiukwaji wa haki za binaadamu vimeripotiwa kufanyika katika maeneo tofauti ya nchi hiyo na kwamba anatarajiwa kutuma msaidi wa katibu mkuu katika masuala ya haki za binaadamu Ivan Simonovic katika mwisho huu wa juma kwa lengo la kwenda kupitia ushahidi wavitendo hivyo. Aidha ameongeza kuwa waliohusika na vitendo hivyo watafikishwa katika mikono ya sheria.
Jeshi la serikali ladhibiti tena eneo la mafuta la Bentiu
Majeshi ya serikali ya Sudan Kusini yalifanikiwa kulirejesha katika himaya yake jimbo lenye utajiri wa mafuta kutoka katika udhibiti wa waasi. Msemaji wa Jeshi Kanali Philip Aguer alisema vikosi vya serikali vilifanikiwa kudhibiti mji wa Bentiu baada ya mapigano ya muda wa masaa mawili na nusu. Aidha afisa huyo wa ngazi ya juu wa jeshi la Sudan Kusini alisema wapiganaji watiifu kwa Machar walikimbia.
Amesema katika maeneo ya mji huo,wapiganaji hao walifanya vitendo vya wizi katika benki, wizi wa vyakula, na kuchoma moto masoko. Na shirika la madaktari wasio na mipaka MSF limesema imeibiwa vifaa vyake katika mji huo wa Bentiu. Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Arjan Hehenkamp amesema si jambo linalokubalika hata kidogo shirika moja na la pekee linalotoa msaada wa kiutu kuibiwa vifaa vyake.
Kulipoteza eneo la Bentiu kutaunyong'onyesha upande wa Machar katika meza ya mazungumzo nchini Ethiopia ambapo wapatanishi wanajaribu kusuluhisha mgogoro huo wa kisiasa ulianza Desemba 15.
Mwandishi: Sudi Mnette AFP
Mhariri: Sekione Kitojo