1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wahimiza kumalizwa mizozo na uchafuzi wa mazingira

20 Septemba 2023

Miito ya kumaliza mizozo na uchafuzi wa mazingira imetawala siku ya kwanza ya mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliofunguliwa Jumanne.

 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Rais Joe Biden wa Marekani akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Picha: Seth Wenig/AP/picture alliance

Katika siku hiyo ya kwanza ya mkutano huo wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa, viongozi waliosimama jukwaani walichagua ajenda wanazozipa kipaumbele, kila mmoja akitumia alau dakika 15 kufafanua masuala ya umuhimu kwa ngazi ya taifa, kikanda na mtizamo jumla wa hali ilivyo duniani.

Rais Joe Biden wa Marekani, ambaye nchi yake ndiyo mwenyeji wa mkutano huo alizungumza saa chache baada ya hotuba ya ufunguzi iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.

Hotuba ya Biden iligusia masuala chungunzima lakini kubwa kuliko yote ni mzozo wa Urusi na Ukraine. Alitumia hotuba yake kutoa mwito kwa viongozi ulimwenguni kusimama pamoja na Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi.

Amesema Urusi inaamini kwamba ulimwengu utaingia woga na kuiruhusu ifanye inavyotaka nchini Ukraine bila kuwajibishwa. Biden akawauliza swali walimwengu, "Je, iwapo tutaruhusu Ukraine isambaratishwe, uhuru wa taifa gani utakuwa salama?"

Rais Joe Biden wa Marekani akitoa hotuba mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa MataifaPicha: Kevin Lamarque/REUTERS

Alishangiliwa kwa makofi aliposema Marekani na washirika wake watasimama imara kuulinda uhuru wa Ukraine na kusisitiza kwamba Urusi peke yake ndiyo inabeba dhima ya vita vinavyoendelea.

Mbali ya suala la Ukraine, kiongozi huyo wa Marekani aligusia masuala mengine, tangu mahusiano ya nchi yake na China, ukosefu wa usalama nchini Haiti, mabadiliko ya tabianchi na mizozo ya kikanda duniani.

Pia aliwakumbusha viongozi wenzake kushikamana kuzikabili changamoto za ulimwengu wa sasa akisema hakuna taifa lenye uwezo wa kushughulikia lenyewe matatizo yote.

Akitumia maneno "maadui wanaweza kuwa washirika, changamoto nzito zinaweza kutatuliwa na vidonda vinaweza kupona", Biden amewatanabahisha viongozi mjini New York kuwa "historia haipaswi kuamua hatma ya walimwengu"

Zelensky ´apigilia msumari´ dhima ya Urusi kwenye mzozo wa Ukraine 

Rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine akitoa hotuba mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa MataifaPicha: Mike Segar/REUTERS

Rais Volodomyr Zelensky wa Ukraine naye alihutubia Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa. Alisimama jukwaani akiwa amevalia mavazi yake yanayomtambulisha tangu kuanza kwa vita. Nayo ni fulana na suruali vyote va rangi ya kijani kikavu.

Kama ilivyotarajiwa,  hotuba yake ilihusu vita vinavyoendelea nchini mwake na kuyahimiza matatifa yote duniani kuiunga mkono Ukraine.

Aliishambulia Urusi kwa kufanya ukatili dhidi ya watoto akisema kinachoendelea ni mauaji ya halaiki. Amesema Urusi pia inatumia chakula na nishati kama ngao za kuitia kishindo dunia ikae kimya kwa uvamizi wake nchini Ukraine.

Aligusia pia suala la kupatikana amani akisema dunia inao wajibu wa kuhakikisha vita vinavyoendelea vinakomeshwa kwa kuzingatia matakwa ya Ukraine na siyo ya Urusi.

Maneno yake yote yaliufikia moja kwa moja ujumbe wa Urusi uliokuwemo ukumbini ukiongozwa na Naibu Balozi wake kwenye Umoja wa Mataifa,  Dmitry Polyansky. 

Rais Vladimir Putin wa Urusi hakuwemo ukumbini kwa sababu mwaka huu hatohudhuria mkutano huo wa mjini New York.

Brazil yajinadi kurejea jukwaa la kimataifa huku Iran ´ikiisuta´ Marekani kuhusu vita vya Ukraine na mkataba wa nyuklia 

Rais Inacio Lula da Silva wa Brazil akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa MataifaPicha: TIMOTHY A. CLARY/AFP/Getty Images

Rais Inacio Lula da Silva wa Brazil alikuwa na ujumbe mmoja tu aliposimama kutoa hotuba. Nao ni kuiarifu dunia kwamba "Brazil imerejea tena kwenye jukwaa la kimataifa".

Amesema nchi yake iko tayari kufanya kazi na Jumuiya ya Kimataifa kutafuta suluhu ya matatizo ya dunia. Hiyo ilikuwa ni hotuba ya kwanza ya Lula tangu alipochaguliwa mwaka jana kuiongoza tena Brazil.

Hotuba yake imetafrisiwa kuwa na lengo la kuachana na sera za mtangulizi wake Jair Bolsonaro aliyejitenga na masuala ya kimataifa.

Rais Ebrahim Raisi wa Iran yeye alizungumzia vita nchini Ukraine kwa kuegemea upande wa Urusi, akiituhumu Marekani kuchochea vita hivyo ili kuyadhoofisha mataifa ya Ulaya. Alisema lakini nchi yake ambayo ni mshirika wa Urusi iko tayari kuona amani inapatikana.

Ama kuhusu mkataba wa nyuklia wa Iran, kiongozi huyo alisema Marekani  haijaonesha nia ya kurejea kwenye mkataba huo wa mwaka 2015 ambao Washington ilijitoa enzi ya rais Donald Trump.

Raisi ameitaka Marekani kuonesha kwa vitendo dhamira yake na Tehran itatimiza wajibu wake.

Mzozo wa Nagorno Karabakh, kitisho cha mabadiliko ya tabianchi na hadhi ya Taiwan vyajitokeza 

Hotuba ya rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki iligusia mzozo wa Azerbaijan na Armenia kuhusu jimbo la Nagorno-Karabakh Picha: TIMOTHY A. CLARY/AFP/Getty Images

Rais Reccep Tayip Erdogan yeye alichagua kuzungumzia kwa upana mzozo wa Armenia na Azerbaijan, akitoa mwito wa kukomeshwa uhasama uliozuka karibuni.

Licha ya kuhimiza kupatikana utulivu, aliikingia kifua Azerbaijan ambayo ni mshirika wa Uturuki. Erdogan alisema anaunga mkono diplomasia kumaliza uhasama uliopo juu ya kuwania eneo la Nagorno Karabakh baina ya maaifa hayo mawili.

Hotuba ya rais wa Colombia, Gustavo Petro, imeitahadharisha dunia kuwa inafanya mchezo na janga la kuongeza kwa joto.

Amesema sayari yetu inajichimbia kaburi yenyewe kwa kupuuza bila kuchukua hatua kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Amekumbusha kwamba muda unayoyoma kuushughulikia mzozo wa hali ya hewa akiutaja kuwa "Zilzala itakayouangamiza ubinaadamu".

Rais Santiago Pena wa Paraguay alichagua mada tete kuipa uzito hotuba yake mbele ya Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa.

Alizungumzia uungaji mkono wa nchi yake wa kuikaribisha Taiwan kama mwanachama kamili wa umoja huo. Paraguay ndiyo nchi pekee ya Amerika ya Kusini inayoitambua Taiwan kidiplomasia.

Kisiwa hicho ambacho China inadai ni sehemu ya himaya yake kilizuiwa kuchukua kiti kwenye Umoja wa Mataifa na mashirika yake mwaka 1971 baada ya kutambuliwa rasmi kwa Jamhuri ya Umma wa China.

Cyril Ramaphosa: Wako wapi wanawake wa sayari yetu?

Baada ya siasa, vita, mabadiliko ya tabianchi na mizozo, ilikuwa ni rais Cryril Ramaphosa wa Afrika Kusini aliyeliliweka mezani suala la kuendelea kuwawezesha wanawake katika kila nyanja duniani.

Ukumbi wa mikutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Alianza hotuba yake kwa swali lililowapata wengi kwa mshangao akiuliza, "wako wapi wanawake wa dunia yetu?"

Yumkini rais Ramaphosa alibaini kwamba yeye alikuwa kiongozi wa 14 kutoa hotuba hapo jana lakini wote walikuwa wanaume.

Hotuba yake ilitoa rai kwa dunia kutowaacha nyuma wanawake, akifafanua mafanikio yaliyopatikana nchini mwake ikiwemo kuwa na Baraza la Mawaziri lenye asilimia 50 ya wanawake. 

Pia aliwaarifu pia viongozi wengine ukumbini, kwamba ujumbe wake wote aliofuatana nao nchini Marekani ulikuwa ni wa wanawake pekee.

Baada ya Ramaphosa akasimama mwanamke wa kwanza kwa mwaka huu kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, naye ni rais Katalin Novák wa Hungary.

Alizungumzia dhamira ya nchi yake kuendelea kuiunga mkono Ukraine akagusia pia masuala ya kuimarisha familia na uhuru wa wazazi katika malezi.

Wanawake wengine waliosimama jukwaani baadaye walikuwa rais Natasa Pirc Musar wa Slovenia na Dina Boluarte wa Peru.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW