1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miito ya kuwafirikia wanafunzi wazazi Tanzania yahanikiza

22 Juni 2021

Wanaharakati wa masuala ya elimu Tanzania wameitaka serikali kuwarejesha shuleni wanafunzi wa kike walioachishwa baada ya kupata ujauzito. Ni baada ya agizo la kuwarudisha wanafunzi wa vyuo vya maendeleo.

Tansania Kondora Mädchenschule
Picha: DW/N. Quarmyne

Hatua hii inakuja ikiwa ni siku moja tu baada ya katibu mkuu wa wizara ya elimu nchini Tanzania, Dk. Leonard Akwilapo kutoa agizo kwa wakuu wa vyuo vya maendeleo ya wananchi akiwataza kuwadahili upya haraka iwezekanavyo wasichana wote waliokatisha masomo kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo ujauzito.

Baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu na masuala ya mtoto wa kike, wamepongeza hatua hiyo, lakini wamesema haitoshi kwa sababu wapo wanafunzi wengine walioacha masomo kwa sababu hizo katika mfumo rasmi wa elimu nao wanapaswa kudahiliwa ili wamalizie masomo yao katika mfumo ulio rasmi.

Soma pia: Wanafunzi wenye mimba wakamatwa Tanzania

Mpango huu wa kuwarejesha wasichana masomoni umekuja baada ya majadiliano ya muda mrefu baina ya serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia ambapo pamoja na masharti mengine waliyoyatoa, lakini pia wanahitaji kuona mtoto wa kike aliekatisha masomo kwa sababu mbalimbali akipewa fursa ya kumalizia elimu yake.

Tangu kuingia madarakani mwezi Machi, rais Samia Hassan Suluhu amebadili mambo kadhaa yalioanzishwa na mtangulizi wake, ambayo watetezi walikuwa wakiyaona kama ya ukandamizaji.Picha: STR/AFP/Getty Images

Hata hivyo msimamo huu laini kuhusiana na mtoto wa kike kurejeshewa haki yake ya kimasomo inakuja ikiwa ni siku chache baada ya Rais mpya Samia Suluhu kuonesha dira tofauti katika baadhi ya misimamo ambayo ni tofauti na ilivyokuwa kwa mtangulizi wake Hayati John Pombe Magufuli ambaye alipinga hadharani msichana kurejea shuleni baada ya kupata ujauzito.

Soma pia: Tanzania na mfumo mpya wa elimu

Betty Masanja, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii anasema kuna umuhimu wapewe nafasi ya kuchagua aina ya mfumo watakaopenda kumalizia elimu yao.

Suala la mtoto wa kike aliyekatisha masomo kupewa nafasi ya pili lilikuwa gumzo katika awamu iliyopita ambapo makundi mbali mbali ya kutetea haki za mtoto wa kike waliibuka na mashinikizo ambayo katika serikali iliyopita hayakuzaa matunda, licha ya baadhi ya wanasiasa kushinikiza banki ya dunia kuiwekea vikwazo vya kimikopo serikali ya Tanzania.

Mwandishi: Hawa Bihoga