1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Mataifa yazungumzia mzozo kati ya Israel na Palestina

9 Oktoba 2023

Mataifa kote ulimwenguni yameendelea kutoa matamko kuhusiana na mashambulizi yaliyofanywa na wanamgambo wa Hamas wa Palestina ambayo Israel imesema yamesababisha vifo vya watu 700.

Mfumo wa kukabiliana na makombora angani wa Israel ukiyadhibiti maroketi yaliyorushwa kutokea Ukanda wa Gaza katika jiji la Ashkelon, Israel Oktoba 8, 2023.
Mfumo wa kukabiliana na makombora angani wa Israel ukiyadhibiti maroketi yaliyorushwa kutokea Ukanda wa Gaza katika jiji la Ashkelon, Israel Oktoba 8, 2023.Picha: Amir Cohen/REUTERS

Matamko ya viongozi wa ulimwengu yanaanzia kulaani vikali huku wengine wakiahidi kuisaidia Israel na wengine wakiipongeza Hamas. Wengi wametoa mwito wa pande zote kusitisha mapigano na hasa baada ya Israel kuanzisha mashambulizi ya angani na operesheni nyingine za kijeshi zinazolenga mamlaka za Hamas.

Tukianzia nchini Marekani, Rais Joe Biden amesema uungaji mkono wa Marekani kwa israel ni thabiti na hautetereki na kuamuru meli za Marekani na ndege za kivita kuisogea Israel. Waziri wa ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin naye akisema, Washington pia itatoa silaha na vifaa kwa Israel.

China imepinga na kulaani machafuko dhidi ya raia nchini Israel na Palestina. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ning amesema China ina wasiwasi mkubwa juu ya machafuko haya ya sasa  na kuongeza kuwa imesikitishwa na kadhia iliyowakumba raia kutokana na mzozo huo. Amesema, China inapinga hatua zinaweza kuchochea kusambaa kwa mzozo na kudhofisha utulivu wa kikanda na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kuhakikisha wanatuliza hali badala ya kuchochea na kuahidi kutoa ushirikiano.

Hata hivyo matamshi hayo yamekosolewa na kiongozi wa walio wengi kwenye Baraza la Seneti la Marekani Chuck Schumer akisema kauli ya China ameyapokea kwa masikitiko kwa kuwa hayakuonyesha huruma wala kuiunga mkono Israel katika kipindi hiki kígumu. Schumer ametoa matamshi hayo alipozungumza na waziri wa mambo ya nje wa China, Wang Yi.

Kansela wa zamani wa Ujerumani Angela Merkel ameungana na mataifa mengine kulaani mashambulizi ya hamas dhidi ya IsraelPicha: Themba Hadebe/AP/picture alliance

Merkel aungana na Scholz kulaani mashambulizi ya Hamas nchini Israel

Katika hatua nyingine aliyekuwa kansela wa Ujerumani Angela Merkel amelaani vikali mashambulizi aliyoyataja kuwa ya kigaidi ya Hamas dhidi ya Palestina. Merkel ameyetaja mashambulizi hayo kuwa ni ya kinyama na kishenzi na kusisitiza kwamba anasimama na watu wa Israel pamoja na serikali ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu.

Merkel aliyehudumu kama kansela wa Ujerumani kwa miaka 16 amesema anaunga mkono kikamilifu matamshi yaliyotolewa na kansela Olaf Scholz jana Jumapili kwamba Israel ina haki ya kujilinda dhidi ya mashambulizi ya kinyama na kuwalinda raia wake.

Huyu hayo yakiendelea, rais wa Iran Ebrahim Raisi amelipongeza kundi la Hamas kwa kile alichokielezea kama ushindi kufuatia mashambulizi hayo makubwa kabisa yaliyofanywa na Hamas, akiyaelezea kama udhihirisho wa "upinzani"

Soma pia: Mzozo kati ya Israel na Hamas wazidi kutokota

"Inadhihirisha upinzani na kusimama dhidi ya utawala bandia wa Kizayuni. Watu wa palestina, wanajeshi wa Palestina, na makundi yote ya Palestina kwa kweli yanatakiwa kupongezwa," alisema Raisi.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis amesema vita na machafuko havitaweza kumaliza mvutano na badala yake husababisha vifo na madharaPicha: The Vatican Media/AFP

Marekani yaonyesha mashaka kufuatia mahusiano kati ya Iran na Hamas

Aidha, Iran imekanusha vikali madai iliyosema hayana msingi kwamba inahusika na mashambulizi hayo huku msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Nasser Kanani akiwaambia waandishi wa habari kwamba madai hayo ni siasa tu na kuongeza kuwa Wapalestina wana uwezo mkubwa wa kulilinda taifa lao na kurejesha haki zao bila hata ya kusaidiwa na Iran.

Soma pia: Baada ya shambulio la Hamas, Netanyahu asema Israel iko vitani

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken alinukuliwa awali akisema ingawa hakuna ushahidi kwamba Iran ilihusika lakini yapo mahusiano ya muda mrefu kati ya Tehran na Hamas. Iran inausaidia mtandao mkubwa wa makundi ya wanamgambo huko Mashariki ya Kati na kuwa na nguvu katika mataifa kuanzia Lebanon, Syria, Iraq na Yemen hadi Gaza kwenyewe.

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imetoa mwito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano na kuhimiza mazungumzo ya kina ili kupatikana suluhu ya muda mrefu na iliyosubiriwa kwa hamu, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wake Maria Zakharova.

Rais wa Ukraine, yeye alisema tu kwamba Israel ina haki isiyopingika ya kujilinda na kuongeza kuwa "ugaidi mara zote ni uhalifu". Rais wa Uganda Yoweri Museveni, kwa upande wake amesema inasikitisha kuona machafuko hayo yameanza upya na kuhoji kwa nini inashindikana kutekelezwa kwa suluhu ya pande mbili?

Soma pia: Biden: Palestina tumieni siasa kupata amani ni Israel

Kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni, Papa Francis amesema jana kwamba ugaidi na vita havisaidii kuleta shuluhu na badala yake husababisha vifo na mateso kwa watu wengi na kutaka watu kuiombea Israel na Palestina.