1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miito yatolewa kutoutanua mzozo wa Mashariki ya Kati

2 Oktoba 2024

Viongozi wa mataifa mbalimbali duniani wameendelea kuzitolea wito Iran na Israel kujizuia na kutoufanya mzozo wa Mashariki ya Kati kuwa mkubwa zaidi.

Beirut I Mwanamke akisoma Quran mbele ya majengo yaliyoharibiwa
Mwanamke akisoma Quran mbele ya majengo yaliyoharibiwa na mashambulizi ya Israel mjini Beirut, LebanonPicha: AFP/Getty Images

Ujerumani imetuma ujumbe kwa ubalozi wa Iran nchini humo na kueleza kuwa inalaani mashambulizi ya jana usiku na kuitaka Tehran kutofanya mashambulizi mengine. Aidha, serikali mjini Berlin imewataka raia wake kuondoka mara moja nchini Iran wakati huu hali ya mvutano ikiongezeka.

Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni ameitisha hivi leo mkutano kwa njia ya video utakaowakutanisha wakuu wa nchi na serikali za kundi la nchi saba zilizostawi zaidi kiviwanda la G7 ili kujadili mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel. Italia imesema itaendelea kufanya kazi ili kuwezesha suluhisho la kidiplomasia katika mzozo huo wa  Mashariki ya Kati.

Israel bado imeshikilia msimamo wake kuwa itajibu mashambulizi hayo ambayo yamesababisha uharibifu katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na mji wa Hod HaSharon. Kwa upande wake Rais wa Iran Massoud Pezeshkian ameionya Israel kuachana na kile alichokiita "vitendo vya uhalifu" au iwe tayari kukabiliana na majibu makali zaidi.

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis ametoa wito wa kufanyika maombi ya amani ifikapo Oktoba 7 mwaka huu, ikiwa ni siku ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu Hamas ilipoishambulia Israel.

Waziri Katz: Guterres hakaribishwi Israel

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Picha: William Volcov/ZUMA Press Wire/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz amemtangaza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuwa mtu asiyetakikana kuonekana ndani ya Israel akimtuhumu kuipinga Israel na kuyapendelea makundi ya kigaidi ya Hamas na Hezbollah. Katz amesema mtu yeyote ambaye hawezi kulaani shambulio baya la Iran dhidi ya Israel, hastahili kukanyaga ardhi ya Israel. Hata hivyo, Guteress amesema:

"Matokeo ya vifo na uharibifu usio kifani huko Gaza sasa yanatishia kulitumbukiza eneo lote kwenye janga la vita kamili ambavyo matokeo yake hayafikiriki. Vita huko Lebanon vinaweza kusababisha mzozo mpana zaidi utakaoyahusisha mataifa yenye nguvu. Ninaunga mkono kikamilifu pendekezo la usitishwaji mapigano litakalowezesha uwasilishwaji wa misaada ya kiutu na kuanza kwa mazungumzo ili kufikia amani ya kudumu."

Soma pia: Hofu yatanda Mashariki ya Kati baada ya mashambulizi ya Iran

Hayo yakiarifiwa, kundi la Hezbollah limesema limekishambulia kikosi cha Israel kwa mabomu karibu na kijiji cha mpakani cha Yaroun kusini mwa Lebanon, wakati wanajeshi wa Israel walipokuwa wakijaribu kuingia nchini humo. Israel imekiri kupoteza wanajeshi sita hadi hivi sasa kutokana na mashambulizi hayo ya Hizbullah.

Kwengineko, vita vya Gaza pia vinaendelea kurindima ambapo mashambulizi ya Israel huko Khan Younis yamesababisha vifo vya Wapalestina 32.

(Vyanzo: Mashirika)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW