1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miito yaongezeka kumtaka Mugabe kuachia ngazi, Zimbabwe

16 Novemba 2017

Raia nchini Zimbabwe wameanza kuangazia mustakabali wa taifa hilo bila ya kiongozi wao aliyekaa madarakani kwa takriban miongo minne, wakati mazungumzo ya maridhiano yakiendelea.

Simbabwe
Picha: DW/C. Mavhunga

Raia nchini Zimbabwe wameanza kuangazia mustakabali wa taifa hilo bila ya kiongozi wao aliyekaa madarakani kwa takriban miongo minne. Jeshi limechukua nafasi ya rais Robert Mugabe mwenye miaka 93, shujaa wa ukombozi aliyegeuka kuwa mtawala wa kiimla, ambaye kwa  sasa yuko katika kizuizi cha nyumbani. zaidi kuhusu kinachojiri Zimbabwe.

Taifa hilo liliachwa na mshangao baada ya rais huyo mkongwe kuwekwa katika kizuizi cha nyumbani jioni ya Jumanne, na wanajeshi kuweka doria kwenye maeneo muhimu  katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare, na maafisa wake waandamizi kutangaza kuchukua udhibiti wa kituo cha televisheni.

Kiongozi wa upinzani aliyerejea nchini humo, Morgan Tsvangira amesema ni lazima rais Robert Mugabe ajiuzulu. Ametaka serikali ya mpito kujadiliwa, na kuhusisha pande zote pamoja na kufanywa mageuzi mapana kabla ya uchaguzi mkuu.

Tsvangirai amewaeleza waandishi wa habari mjini Harare kwamba kunatakiwa kuwepo na mkakati wa baada ya kufanyika kwa uchaguzi ili kuhakikisha utulivu, na mkakati huo usimamiwe na jumuiya ya maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC na Umoja wa Afrika, AU.

Makamu wa rais aliyefutwa kazi mwaka 2014 Joice Mujuru kwa upande wake ametoa mwito wa kufanyika uchaguzi huru na wa haki, wakati mchakato wa kuundwa kwa serikali ya mpito  ukiendelea na kuhusisha pande zote. Mujuru alifutwa kazi na rais Robert Mugabe kwa madai ya kupanga mikakati ya kuwania nafasi ya uraia.

Joice Mujuru, aliyewahi kuwa makamu wa rais wa Robert Mugabe ataka kuondolewa kwa upendeleo kwa raia nchini humo.Picha: DW/A.MacKenzie

Makundi ya kiimani na haki za binadamu yataka utulivu.

Kwa upande mwingine, kampeni iliyonzishwa na mchungaji Evan Mawarire kupitia mtandao wa kijamii yenye hashtag #ThisFlag Movement imeibua maandamano makubwa yanayoipinga serikali ambayo hayajatokea katika kipindi cha muongo mmoja, na inataka raia kuhakikisha  amani inasalia nchini humo.

Vyama vya upinzani, asasi za kiraia na makundi ya kiimani yametaka utulivu na kuheshimiwa kwa haki wakati mazungumzo yakiendelea ili kutatua mzozo uliopo na ambayo labda yatakayofikisha hatma ya utawala wa muda mrefu wa rais Robert Mugabe. Zaidi ya asasi 100 za kiraia yanataka Mugabe kuachia madaraka kwa amani.  

Mawaziri kutoka mataifa wanachama wa Jumuiya ya uchumi kwa nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, chini ya uenyekiti wa Afrika Kusini na Angola, wanakutana leo hii nchini Botswana kujadili sintofahamu hiyo, na mapendekezo yao yatawasilishwa kwa wakuu wa nchi na serikali.

Ubalozi wa Marekani umewataka raia kujiepusha na mizunguko isiyo ya lazima, wakati ambapo hali nchini humo bado ni tete. Serikali ya Uingereza, yenyewe imewataka raia wake waliopo, Harare kujiepusha na mikusanyiko na maandamano yoyote.

Si Mugabe wala mkewe, Grace ambao wamezungumza chochote tangu kuanza kwa operesheni hiyo ya kijeshi. Lakini Wazimbabwe wengi wanataraji kwamba mzozo huo utafungua njia ya maisha bora zaidi huko mbele.

Msemaji wa chama tawala, ZANU-PF, Simon Khaya Moyo, amesisitiza kwamba hili ni suala la kawaida. Raia wamepuuzia uwepo wa wanajeshi kwenye mitaa ya mji wa Harare na kuendelea na shughuli zao, huku wachambuzi wakielezea kwamba kuna uwezekano kuwa Mugabe na jeshi wanajadiliana kuhusu serikali ya mpito.

Rais Mugabe, mkewe Grace na washirika waandamizi wa kisiasa wanazuiwa nyumbani, katika kasri la Mugabe maarufu "Blue House”, mjini Harare, kimesema chanzo kimoja cha kisiasa.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/EAP/DRINGEND

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

   

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW