Miji mikubwa Iran yakumbwa na maandamano
17 Novemba 2019Katika ghasia hizo inaripotiwa kuwa kiasi mtu mmoja ameripotiwa kuuwawa.
Maandamano hayo yameweka mbinyo mpya dhidi ya serikali ya Iran wakati ikihangaika kuondokana na vikwazo vya Marekani vinavyoikaba nchi hiyo baada ya rais Donald Trump wa Marekani kuitoa nchi hiyo kutoka katika makubaliano ya kinyuklia kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani.
Katika maandamano ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa ya amani , maandamano yaligeuka kuwa ya ghasia katika maeneo kadhaa, ambapo vidio zilizowekwa katika mtandao zilionesha polisi wakifyatua mabomu ya gesi ya kutoa machozi na makundi ya watu yakiwasha moto. Wakati yakiwakilisha kitisho cha kisiasa kwa rais Hassan Rouhani kabla ya uchaguzi wa bunge mwezi Februari, pia yanaonesha ghadhabu ilisosambaa kwa watu wengi miongoni mwa Wairan milioni 80 ambao wameshuhudia hifadhi yao ya fedha ikiyeyuka kutokana na ukosefu wa ajira na kuporomoka kwa sarafu ya taifa hilo ya rial.
Maandamano yalifanyika katika miji zaidi ya 12 katika muda kufuatia uamuzi wa Rouhani mapema siku ya Ijumaa kupunguza ruzuku katika mafuta ili kugharamia fedha zitolewazo kwa watu masikini nchini humo. Mafuta nchi humo bado yanabaki kuwa rahisi duniani, ambapo bei mpya imepanda hadi rial 15,000 kwa lita moja, ikiwa ni ongezeko la asilimia 50 kutoka siku moja kabla. Hii ni senti 13 kwa lita, ama kiasi ya senti 50 kwa galoni moja. Galoni ya mafuta ya kawaida nchini Marekani ni kiasi ya dola 2.60, ukilinganisha.
Mafuta bado ni bei ya chini
Lakini katika taifa ambako wengi wanaendesha maisha yao kama madereva wa teksi ambao sio rasmi, mafuta rahisi yanaonekana kuwa haki ya kuzaliwa. Iran ni nchi ya nne duniani yenye hazina kubwa ya mafuta ghafi. Wakati ikitarajiwa kwa miezi kadhaa, uamuzi huo bado umewafikia watu wengi bila ya kutarajia na kuzusha ghafla maandamano.
Ghasia zilizuka siku ya Ijumaa usiku katika mji wa Sirjan, ulioko kilometa 800 kusini mashariki mwa tehran. Shirika la habari la nchi hiyo IRNA limesema, waandamanaji walijaribu kuchoma moto kituo cha kuhifadhi mafuta, lakini walizuiwa na polisi.
Polisi hawakutoa taarifa zaidi, lakini vidio zilizowekwa mtandaoni nchini Iran zinaonesha moto katika kituo hicho cha kuhifadhi mafuta wakati magari ya polisi yakisikika. Vidio nyingine inaonesha kundi kubwa la watu likipiga kelele: Rouhani, aibu kwako ! Ondoka nchini peke yako !"
Mohammad Mahmoudabadi, afisa wa wizara ya mambo ya ndani katika mji wa Sirjan, baadaye aliimbia televisheni ya taifa kuwa polisi na waandamanaji walishambuliana kwa risasi, na watu kadhaa kujeruhiwa. Amesema mandamanaji mengi yalikuwa ya amani, lakini baadaye watu waliojifunika nyuso zao wakiwa na bunduki na visu walijiingiza katika maandamano hayo.