1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miji ya kusini mwa Ukraine yashambuliwa na Urusi

2 Aprili 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewaonya watu wake kuwa wanajeshi wa Urusi wanaoondoka wanatengeneza "mazingira ya maafa" nje ya mji mkuu kwa kutega mabomu ya ardhini karibu na nyumba za watu na maiti

Ukraine | Zerstörung in Mariopol
Picha: ALEXANDER ERMOCHENKO/REUTERS

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewaonya watu wake mapema leo kuwa wanajeshi wa Urusi wanaoondoka katika maeneo yao wanatengeneza kile amesema ni "mazingira ya maafa" nje ya mji mkuu kwa kutega mabomu ya ardhini katika eneo zima hata karibu na nyumba za watu na maiti. Ametoa onyo hilo wakati mzozo wa kiutu katika mji uliozingirwa wa Mariupol ukitokota. Wanajeshi wa Urusi walizuia operesheni za kuwahamisha watu kwa siku ya pili mfululizo hapo jana. 

Mapambano yaendelea Mariupol

Katika mji wa kusini wa Mariupol, wakaazi waliofanikiwa kukimbia mashambulizi ya makombora kwa wiki kadhaa walisimulia uharibifu mkubwa waliouacha nyuma. Wanasema mji huo sasa ni kaburi la pamoja kwa kila mtu. Takribani watu 160,000 bado wamenasa Mariupol, wakisubiri msaada kwa sababu hawana maji, chakula wala umeme.

Rais Zelensky alikutana Kyiv na Rais wa Bunge la Ulaya Roberta Metsola Picha: Ukrainian Presidential Press Office/AP/picture alliance

Askari wa Urusi wameuzingira Mariupol katika jaribio la kuukamata mji huo ili kuunganisha na maeneo yaliyojitenga katika mikoa ya Lugansk na Donetsk chini ya askari wanaoungwa mkono na Moscow katika upande wa mashariki na rasi ya Crimea, ambayo iliikwapua mwaka wa 2014.

Soma pia: Ukraine yatuma msafara wa mabasi kuondoa watu Mariupol

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, ambalo timu yake ya wahudumu tisa katika magari matatu walikuwa njiani kwenda mjini humo kusaidia kuratibu operesheni ya uokozi, walisema walishindwa kufika Mariupol wala kusimamia uhamishwaji salama wa raia. Taarifa imesema watajaribu tena leo.

Shambulizi la kwanza kwenye ardhi ya Urusi

Moscow imeituhumu Kyiv kwa kufanya shambulizi lake la kwanza la kutokea angani kwenye ardhi ya Urusi, ikiwa ni pigo kubwa katika matumaini ya juhudi zozote za kuutuliza mzozo katika vita vya Rais Vladmir Putin dhidi ya Ukraine.

Mazungumzo ya amani kati ya maafisa wa Ukraine na Urusi yaliendelea jana kwa njia ya video, lakini Moscow ilionya kuwa shambulizi hilo la helikopta kwenye ghala la Mafuta katika mji wa Belgorod lingeweza kuathiri mazungumzo hayo. Kyiv haikukiri waka kukanusha kuhusika na shambulizi hilo, huku Waziri wa Mambo ya Kigeni Dymitro Kuleba akisema hakuwa na taarifa zote za kijeshi.

Mazungumzo yamekwama baina ya Ukraine na Urusi

01:18

This browser does not support the video element.

Kwenye uwanja wa mapambano, wanajeshi wa Ukriane walianza kuchukua tena udhibiti wa baadahi ya maeneo yakiwemo ya karibu na mji mkuu Kyiv na eneo la kusini la Kherson – mji pekee muhimu ambao Urusi ilikuwa imeukamata.

Soma pia: Urusi yatishia kusitisha usambazaji gesi Ulaya

Warusi waendelea kuondoka

Wizara ya ulinzi ya Ukraine imesema wanajeshi wa Urusi wanaendela kuutekeleza mpango wao wa kuondoka katika baadhi ya maeneo kuanzia kaskazini mwa Kyiv kueleeka mpaka wa Belarus. Raia wanaendelea kuondoka katika maeneo yaliyoharibiwa kwa vita wakati askari wa Ukraine wakivikomboa vijiji 11 katika maeneo ya karibu na Kyiv na Cherginiv katika upande wa kaskazini.

Umoja wa Ulaya umeigeukia China, kwa kuionya Beijing katika mkutano wa kilele kwa njia ya video kutoegemea upande wa Urusi. Rais wa Halmashauri kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema China iliarifiwa kuwa uungwaji mkono wowote wa vita vya Urusi utasababisha uharibifu mkubwa wa sifa barani Ulaya. Von der Leyen na Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel walizungumza na Waziri Mkuu wa China Li Keqiang na Rais Xi Jinping jana. Beijing inaiunga mkono kisiasa Urusi na imekataa kulaani uvamizi huo, ikielezea sera ya Marekani na Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuwa sababu kuu za mzozo huo.

Mwandishi: Bruce Amani

Reuters, ap, afp, dpa

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW