Mikakati ya Tanzania kupunguza maambukizi ya HIV
1 Desemba 2021Ndani ya kipindi cha miaka 38 tangu janga hilo la maambukizi ya virusi vya Ukimwi kuripotiwa kwa mara ya kwanza nchini Tanzania, juhudi za kukabiliana na kuenea kwake, zinatajwa kuzaa matunda huku takwimu zikionyesha wastani wa maambukizi mapya umepungua maradufu.
Kulingana na takwimu zilizotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani, ingawa Tanzania inajihesabu kufauli kupunguza kiwango cha maambukizi hayo, lakini inahisi kuathiriwa na maambukizi mapya yanayoendelea kuitikisa dunia, yaani tatizo la covid-19.
Amesema wakati dunia ikiendelea kukuna vichwa namna ya kukabiliana na mlipuko mwingine wa maambuziki ya virusi vya corona, Tanzania itaendelea kutumia rasilimali zake za ndani pamoja na zile za wahisani kuongeza nguvu ya utoaji elimu kwa wananchi ili kudhibiti maambukizi hayo.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa katika kipindi cha mwaka 2016-2017 maambukizi ya VVU kwa watu wenye umri wa miaka kuanzia 15 hadi 49 yalikuwa ni asilimia 4.7 yakiwa yameshuka ikilinganishwa na yale yaliyorekodiwa mwaka 2011-2012 yaliyokuwa asilimia 5.1.
Hata hivyo, baadhi ya maeneo kiwango cha maambukizi kinaonekana kusalia kuwa juu wakati jiji la Dar es salaam ambalo limekuwa likiongoza kupokea wageni wengi wa ndani ya nje, haliko katika mikoa 14 inayoongoza kwa kuwa na maambukizi ya kiwango cha juu.
Ili kuzidisha msukumo katika vita ya kukabiliana na maambukizi hayo, serikali imeanisha mikakati kadhaa ikiwamo ile ya upanuaji wa utoaji elimu kuanzia ngazi ya elimu ya msingi hadi ngazi za juu.
Kama hiyo haitoshi, mpango wa kuwahamasisha wanaume kufanya tohara kama sehemu ya kupunguza maambukizi nao unatarajiwa kupewa kipaumbele ambapo kampeni mbalimbali zinatarajiwa kuendeshwa kuwaraia wanaume kuitikia mwito huo kwa hiari yao.
Mpango wa usambazaji wa dawa zinazotumika kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi yaani ARV, umesaidia kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi hivyo na serikali inasema wale wanaoendelea kujitokeza kupima na kisha kutambua hali ya afya zao wanapewa kipaumbele kupewa dawa iwapo wanagundulika kupata maambukizi.