1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mikataba ya Geneva yatimiza miaka 70

Daniel Gakuba
12 Agosti 2019

Ni miaka 70 leo tangu kusainiwa kwa mikataba minne ya Geneva, iliyoweka msingi wa sheria ya kimataifa ya kulinda haki za binadamu. Lakini ingawa nchi 196 zimeitia saini mikataba hiyo, utekelezwaji wake unasuasua.

Schweiz | Genfer Konvetionen (ICRC Archives (ARR)/J. Cadoux)
Picha: ICRC Archives (ARR)/J. Cadoux

 

Mikataba hiyo minne ya baada ya vita vikuu vya pili iliweka kanuni za kulinda haki za raia na wanajeshi katika mazingira ya vita. Ingawa nchi 196 ni wanachama wa mikataba hiyo, utekelezwaji wake wakati huu unakabiliwa na kitisho katika maeneo kadhaa ya mizozo. 

Kwa mujibu wa mikataba hiyo na itifaki kadhaa za nyongeza, raia na wanajeshi wanayo haki ya kutendewa ubinadamu katika mizozo ya kivita, na mashambulizi yoyote ya kijeshi yanaruhusiwa tu dhidi ya shabaha za kijeshi. Lakini, wakati mizozo ya kisasa ikijikita zaidi katika mazingira ya mjini, pande zinazohasimiana zimekuwa mara kwa mara zikiikiuka mikataba ya Geneva.

Soma zaidi: Saudi Arabia kikaangoni juu ya rekodi yake ya haki za binadamu 

Mashambulizi yaliyoibuka upya dhidi ya raia nchini Syria, mamia ya raia wanaouawa nchini Afghanistan, Shirika la kimataifa la Msalaba mwekundu linasema mikataba ya Geneva haionekani kuzia unyama wa kivita kama inavyopaswa.

Syria, mfano hai wa uvunjifu wa mikataba ya Geneva

Nakala ya mojawapo ya mikataba minne ya Geneva iliyotiwa saini Agosti 12, 2019Picha: ICRC Archives (ARR)

Mkururgrnzi mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, Kenneth Roth anasema ukiukaji wa mikataba hiyo umeenea kutoka Myanmar, Yemen hadi Syria.

''Kuwepo kwa mikataba hiyo hakuna maana kwamba inaheshimiwa na kila upande. Leo hii ukiukwaji wake unaonekana dhahiri katika vita vya Syria. Vikosi vya rais Bashar al Assad kwa kusaidiwa na Urusi huwalenga kwa makusudi raia na taasisi za kiraia katika maeneo yanayodhibitiwa na wapizani.'' Amesema Roth.

Lakini mkurugenzi anayehusika na sheria za kibinadamu katika shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu Helen Durham, anasema kukiuka kwa mikataba hiyo hakuondoi umuhimu wake.

Amesema, ''Kila mara tunasikia na kuona katika vyombo vya habari, visa vya kutisha vya ukiukaji wa sheria za kivita, raia wakishambuliwa, na wafungwa wa kivita wakivunjiwa heshima ya utu wao, zipo sehemu nyingine nyingi ambako mikataba hiyo bado inalinda heshima ya ubinadamu katika mizozo ya vita.''

Bado sheria hizo zinakwenda na wakati

Peter Maurer, Rais wa Shirika la Kimataifa la Msalaba MwekunduPicha: Reuters/D. Balibouse

Hata rais wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu Peter Maurer alisema hivi karibuni, kwamba visa vya ukiukwaji wa mikataba ya Geneva ni vichache ikilinganishwa na inavyozingatiwa. Ametoa mfano akisema, pale watoto walio katika msitari wa mbele wa vita wanaporuhusiwa kuondoka, au majeruhi wanaporuhusiwa kupita katika vizuizi vya barabarani na kupelekwa mahali wanapoweza kutibiwa, yote hayo yanatokana na mikataba hiyo.

Anasema kabla ya kusainiwa kwa mikataba hiyo mwishoni mwa vita vikuu vya pili, raia hawakuwa na sheria ya kimataifa ya kuwalinda, na mamilioni waliuawa barani Ulaya na kwingineko.

Soma zaidi: UNHRC yataka wakuu wa kijeshi Myanmar washtakiwe

Nchi 196, ikiwa ni pamoja na wanachama wote wa Umoja wa Mataifa, kujumuisha wanachama waangalizi kama Palestina, zimeitia saini mikataba ya geneva iliyoidhinishwa tarehe 12 Agosti mwaka 1949.

Rais wa Shirika la Msalaba Mwekundu anasema miaka 70 baadaye, leo hii mikataba hiyo bado inaendana na wakati na haihitaji mabadiliko yoyote, bali shinikizo la kisiasa kwa wanachama wake wote kuiheshimu ipasavyo.

DW

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW