Mikoko hatarini kutoweka Tanzania
19 Septemba 2018Tahadhari hiyo ilitolewa na wataalamu wa misitu walpokutana jijini Dar es Salaam kujadili namna ya kuinusuru misitu ya mikoko, ambao walioonya kuwa kasi ya ongezeko la idadi ya watu inayoegemea mavuno ya kasi ya misitu hiyo ni chanzo kikubwa cha kutoweka kwake.
Mikoko ni aina ya misitu inakatwa kiharamu kwa kasi zaidi hata kutishia kutoweka kwake, ikiwemo mikoko aina ya Heritiera litoralis, hii imevunwa kupita kiasi katika Delta ya Rufiji.
Wataalamu wa aina hiyo ya misitu nchini Tanzania wanatoa tahadhari ya wazi kwa mamlaka husika kuhakikisha zinakabiliana na uvunaji haramu wa aina hiyo ya misitu inayotegemewa kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.
Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la linalojihusisha na utunzaji wa misitu aina ya mikoko la Wetlands, Julii Mulonga, anasema kuwa wananchi wengi hukata misitu hiyo kutokana na kutojuwa umuhimu wake, huku hali ikiwa ni mbaya zaidi itakayogharimu kiasi kikubwa cha fedha katika kurejesha uasili wa misitu hiyo.
Mkataba wa RAMSA uliosainiwa na mataifa mbalimbali yaliyo katika maeneo owevu, yakiwemo maeneo ya mikoko inayopatikana ukanda wa pwani ya Tanzania, unakata uvunwaji holela wa misitu ya mikoko upigwe marufuku.
Mkataba huo unataka wananchi washauriwe kutafuta shughuli zingine za kiuchumi ili kupunguza utegemezi wa aina hiyo ya misitu.
Wakala wa huduma za misitu nchini Tanzania unabainisha kuwa mwaka 1991 nchi hiyo ilikuwa na hekta 115,000 za misitu ya mikoko inayoambaa kaskazini mwa Tanzania na Kenya hadi katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji, lakini hadi kufikia mwaka huu wanaimani mikoko hiyo huenda ikawa imepungua kutokana kuongezeka kwa idadi ya watu halkadhalika shughuli za binaadamu katika maeneo ya hifadhi ya misitu hiyo.
Zawadi Mbwambo, mkurugenzi wa usimamizi wa mali za misitu kutoka wakala wa huduma za misitu Tanzania, anasema wanakabiliana na changamoto lukuki katika kudhibiti upatikanaji haramu wa misitu hiyo.
Kuwapatia elimu wananchi, kuongeza doria pamoja na serikali kutoa mbinu mbadala za shughuli za kiuchumi kunatajwa huenda ikawa ni sehemu ya mbinu ya kukomesha uvunwaji wa misitu ya mikoko ambayo ni sehemu ya mazalia ya samaki na viumbe wengine baharini.
Mwandishi: Hawa Bihoga/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman