1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Milio ya risasi imesikia karibu na makazi ya rais Niger

Daniel Gakuba
31 Machi 2021

Wakaazi wa mji mkuu wa Niger, Niamey wamesema wamesikia milio ya risasi katika maeneo yanayoizunguka Ikulu ya rais usiku wa kuamkia leo (31.03.2021)

 Nigeria Idrissa Waziri Sprecher des neu gewählten Präsidenten Mohammed Bazoum
Picha: Hamid Ngadé

Simulizi za wakazi wa Niamey waliosikia milio hiyo ya binduki, zinasema ufyatuaji huo wa risasi ulianza majira ya saa tisa usiku na kuendelea kwa muda wa kati ya dakika 15 na 20. Mashahidi waliozungumza na shirika la habari la AFP wamesema kuwa mwanzoni wamesikia mchanganyiko wa milio ya silaha nzito na nyepesi, na kwamba kadri muda ulivyosonga mbele, silaha nzito zilinyamaza, zikabakia nyepesi tu.ba

Kulingana na wakaazi hao, milio hiyo ya silaha ilisikika katika wilaya ya Plateau yalipo makaazi rasmi ya rais pamoja na ofisi yake.

Gazeti moja la mtandaoni la Actuniger.com limeripoti kuwa ilipotimia saa kumi alfajiri, hali ya utulivu ilikuwa imerejea mjini Niamey. Mkanda wa vidio ulisambaa katika mitandao ya kijamii ukionyesha mioto ya zana za kijeshi katika giza totoro la mji huo mkuu, lakini haikuwezekana kubainisha mahali wala muda mkanda huo wenye urefu wa sekunde kadhaa uliporekodiwa.

Wanajeshi kadhaa wametiwa mbaroni kufuatia mkasa huo.

Vikosi vya kutuliza ghasia vya Niger, mjini NiameyPicha: Reuters TV/REUTERS

Chanzo kimoja cha kijeshi kimearifu kuwa wanajeshi kadhaa wamekamatwa kuhusiana na mashambulizi hayo wakituhumiwa kujaribu kuiangusha serikali, na kuongeza kuwa hadi sasa vyombo vya usalama vinaidhibiti hali ya mambo.

Aidha, chanzo hicho ambacho hakikutaka jina lake litajwe, kimeendelea kueleza kuwa kikosi cha walinzi wa rais kilingilia kati, na kulizuia kundi la wanajeshi waasi lililokuwa likitaka kuisogelea Ikulu ya rais.

Hiki kinachoelezwa kuwa jaribio la mapinduzi kimekuja siku mbili tu kabla ya kuapishwa rais mteule wa nchi hiyo Mohammed Bazoum, ambapo atakapoanza majukumu yake Ijumaa ijayo atakuwa kiongozi wa kwanza wa Niger kukabidhiwa madaraka na mtangulizi wake kwa njia ya amani, tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1960.

Bazoum aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, ni mshirika wa karibu wa rais Mahamadou Issoufou ambaye anang'atuka mamlakani baada kuhudumu kwa mihula miwili.

Ushindi wake katika duru ya pili ya uchaguzi ya tarehe 2 Februari ulithibitishwa na korti ya katiba mapema mwezi huu wa Machi, lakini unaendelea kupingwa na mpinzani wake Mahamane Ousmane, ambaye anadai kuwa ndie alikuwa mshindi halali.

Chanzo: afpe, ape

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW