1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Milio ya risasi inaendelea kusikika nchini Sudan

19 Aprili 2023

Miripuko iliutikisa mji mkuu wa Sudan, Khartoum jioni ya Jumanne licha ya upande mmoja kudai kusitisha mapigano yaliodumu kwa siku ya nne ambayo yamesababisha vifo vya karibu watu 200

Sudan Kämpfe/Haus in Khartoum
Picha: REUTERS

Mapambano ya muda wa wiki moja ya kuwania madaraka, Jumamosi iliyopita yalizusha mapigano kati ya vikosi vya majenerali wawili walionyakua mamlaka katika mapinduzi ya 2021, yaani mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na naibu wake, Mohamed Hamdan Dagalo, ambaye anaongoza Kikosi cha Msaada wa Dharura (RSF).

Tangu wakati huo, wito wa kimataifa umeongezeka wa kukomesha uhasama ambao umesababisha kuongezeka kwa uasi, vifo na uharibifu. Kamanda wa RSF Dagalo, anayejulikana kama Hemeti, alitangaza kuunga mkono jitihada ya kimataifa ya kusitisha mapigano kwa masaa 24 huku upande wa jeshi la Sudani ukionekana kama kutotilia maanani jambo hilo.

Milio ya risasi katika mji mkuu Khartoum na miji mingine

Kwa mujibu wa mashuhuda kadhaa hadi nyakati za jioni muda ambao ulitarajiwa kuanza usitishwaji wa mapigano, milio ya risasi bado iliendelea kusikika katika mji mkuu wa Khartoum, na iliendelea hadi jioni. Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amenukuliwa akisema "Hadi sasa mapigano nchini Sudan, ikiwa ni pamoja na Khartoum na maeneo mengine mbalimbali. Hakuna dalili ya kusitishwa kwa mapigano." Alisema afisa huyo.

Tangazo la Dagalo lilitolewa baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kusema alizungumza na majenerali hao wawili na kusisitiza haja ya dharura ya kusitishwa kwa mapigano. Awali Jumanne hiyohiyo mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa yenye nguvu ya kiuchumi duniani G7, ambayo ni pamoja na Marekani, pia yalikuwa wametoa wito kwa pande zinazozozana kumaliza uhasama mara moja, katika kipindi mabacho pia miripuko mikubwa ilikuwa ikiendelea kusikika mjini Khartoum, ambapo wanamgambo waliovalia vilemba walitanda mitaani.

Ushahidi wa matukio ya uvamizi katika taasisi za kimataifa

Ikisisitiza uwepo wa machafuko hayo, Serikali ya Washington ilisema moja ya misafara yake ya kidiplomasia kushambuliwa, na Umoja wa Ulaya ulisema nyumbani kwa balozi wake kulifanyiwa mashambulizi. Makundi ya misaada ya kiutu yameripoti  uporaji wa vifaa vya matibabu na nyenzo nyingine.

Wakazi wa mji mkuu waliojawa na hofu wanatumia siku za mwisho za mwezi wa Ramadhani huku kukiwa na mitetemeko yamajengo iliyosababishwa na  vifaru mitaani huku moshi ukifuka kutokana na miripuko ya majengo na maeneo mengine.

Juhudi ya utaoji wa misaada ya kiutu inakabiliwa na mapambano

Mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths amesema wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu na vifaa vinaendelea kulengwa katika makabiliano ya Sudan.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter kiongozi huyo amesema Umoja wa Mataifa umekuwa ukipokea taarifa kwamba kumekuwa na mashambulizi na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wafanyakazi wa misaada ya kiutu.

Soma zaidi:Msafara wa ubalozi wa Marekani washambuliwa Sudan

Katika taarifa yake hiyo aliongeza kuandika kuwa kulikuwa na vitendo vya uporaji katika ofisi ya misaada ya Umoja wa Mataifa huko Kusini mwa Darfur.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW