Milipuko Burundi: Watu 13 wafariki na 57 wajeruhiwa
2 Aprili 2026
Taarifa hiyo imetolewa Jumatano jioni na msemaji wa jeshi la Burundi Jenerali Gaspard Baratuza aliyethibitisha taarifa za awali kuwa moto huo uliozuka kuanzia saa moja usiku wa Jumanne katika ghala la kuhifadhia vifaa vya kijeshi, ulitokana na hitilafu za umeme na hivyo kusababisha milipuko kadhaa ya risasi na mabomu. Jenerali Baratuza amesisitiza kuwa hakukuwa na shambulio lolote dhidi ya kambi hiyo.
Tukio hilo lilitokea katika eneo la Musaga , kusini mwa jiji la Bujumbura, ambapo wakazi walikimbia kwa hofu huku milipuko ikisikika kwa umbali mkubwa huku maafa yakishuhudiwa pia katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo.
Tamko la jeshi la Burundi kuhusu mkasa huu
Msemaji wa jeshi la Burundi ametoa idadi ya awali ya waliofariki na kujeruhiwa kutokana na mkasa huo na amesema milipuko kutokana na moto huo ilisababisha maafa na uharibifu mkubwa wa vifaa.
"Raia kumi na watatu wamefariki. Watu hamsini na saba wamejeruhiwa, wakiwemo raia 54 na wanajeshi watatu. Nyumba kadhaa ziliharibiwa katika vitongoji mbalimbali pamoja na magari ya watu binafsi. Pia vifaa vya kijeshi viliteketea kwa moto na kuharibiwa," alisema Jenerali Baratuza.
Moto huo pia ulisababisha kukatika kwa umeme katika kambi hiyo inayofahamika kama "Base" na vitongoji vyake, ambapo wakazi wa maeneo ya Gasekebuye, Kanyosha, Kinindo na kwengineko walitakiwa kutokuwa na hofu. Hali ya utulivu imerejea mjini Bujumbura baada ya taharuki kufuatia milipuko hiyo huku mamlaka zikieleza kuwa watoto waliokimbia wakiwa peke yao wakati wa tukio hilo sasa wapo katika Parokia ya Kanisa Katoliki ya Buhonga wakisubiri kukutanishwa tena na familia zao.
Kauli za baadhi ya wakazi na viongozi
Idrissa Mbazumutima ni mkaazi na mjasiriamali mjini Bujumbura ameelezea hali ilivyo siku ya Alhamisi kuwa watu wameendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu kutokana na ufafanuzi wa kilichotokea uliotolewa na jeshi la polisi huku akiamini kuwa kila kitu kipo chini ya udhibiti ili kuzuia kosa kama hilo kutokea tena.
Hata hivyo, Gavana wa jiji la Bujumbura Meja Jenerali Aloys Ndayikengurukiye, amewahimiza wananchi kuripoti vitu vyoyvote vinavyotiliwa shaka huku jeshi likiwahimiza kutoa taarifa mara moja kuhusu silaha zozote ambazo hazijalipuka ili ziweze kuondolewa salama na kuepuka kuzigusa kabisa.
Msemaji huyo wa jeshi Jenerali Gaspard Baratuza, amehitimisha kwa kusema kuwa licha ya uharibifu mkubwa wa vifaa na zana za kijeshi, nchi ya Burundi imejizatiti na mifumo yake ya ulinzi bado ipo imara ili kuhakikisha amani na usalama wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.