1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Milipuko yaendelea Sudan huku vita vikiingia mwezi wa pili

16 Mei 2023

Mapigano makali yameendelea kote katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum mapema leo, mnamo wakati jeshi likijaribu kulinda kambi zake muhimu kutokamatwa na kikosi chenye nguvu cha wanamgambo, RSF.

Sudan Khartum Kämpfe Bürgerkrieg
Picha: Mohamed Nureldin/REUTERS

Mashambulizi ya angani na ufyatuaji wa mizinga, vyote vimerindima katika mitaa kadhaa ya mji wa Khartoum mapema leo, kwenye machafuko ambayo yameingia mwezi wa pili sasa.

Kulingana na mashuhuda mashambulizi hayo ya angani yamesikika pia kusini mwa Khartoum, na miripuko mikubwa kutokea kote karibu na Mto Nile ikiwemo miji inayopakana nayo kama Bahri na Omdurman.

Mapigano hayo kati ya pande mbili zinazohasimiana, jeshi la taifa likiongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na kikosi chenye nguvu cha wanamgambo wa Rapid Support (RSF) kinachoongozwa na naibu wa zamani wa mkuu wa majeshi jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, yanafanyika sana mjini Khartoum lakini yamesababisha pia machafuko katika maeneo mengine ya Sudan hususan jimbo la magharibi Darfur.

Machafuko yatishia mgogoro wa kibinadamu

Yamesababisha mgogoro wa kibinadamu unaotishia kuyumbisha kanda hiyo. Tayari zaidi ya watu 700,000 ni wakimbizi wa ndani nchini Sudan na takriban 200,000 wamekimbilia nchi jirani.

Takriban raia 700,000 wa Sudan ni wakimbizi wa ndani na wanahitaji misaada ya kiutu.Picha: Ibrahim Mohammed Ishak/REUTERS

Sudan yageuka uwanja wa mapigano kwa wapiganaji wa kigeni

Ayman Hassan, mwenye umri wa miaka 32 ambaye ni mkaazi wa Khartoum amesema hali inazidi kuwa mbaya. Walikimbia makwao wakaenda kwa jamaa yao mmoja Khartoum, lakini sasa mashambulizi yanawafuata kila wanapoenda hadi mitaani. "Hatujui kile raia walifanya hata wakakabiliwa na vita hadi kwenye majumba”. Ameongeza kusema.

Mapambano yameongezeka mjini Khartoum na Geneina, mji mkuu wa jimbo la Darfur Magharibi, tangu pande mbili kwenye mzozo huo zilipoanza mazungumzo ya amani mjini Jeddah Saudi Arabia wiki moja iliyopita, kufuatia ushawishi wa Marekani na Saudia.

Wanamgambo wa RSF walishutumu jeshi kushambulia hospitali

Kwenye mazungumzo hayo, wajumbe wa majadiliano walikubaliana kuruhusu misaada ya kiutu kusafirishwa ili kuwafikia waathiriwa wa mapigano. Aidha walikubaliana kulinda raia. Lakini hawajaafikiana kuhusu taratibu za kutumika kusafirisha misaada hiyo ya kiutu na vilevile usitishaji vita.

Mbinu za jeshi na RSF kwenye mapambano yao

Jeshi limekuwa likitegemea pakubwa operesheni ya angani kwenye mashambulizi yake. Linashiriki kwa nadra sana mapigano ya ardhini dhidi ya wanamgambo wa RSF ambao wamechukua udhibiti wa baadhi ya mitaa ya Khartoum, tangu machafuko yalipoanza Aprili 15.

Wakaazi na mashuhuda wamesema mapema leo Jumanne, wanamgambo wa RSF walishambulia kambi kuu za kijeshi zilizoko kaskazini mwa Omdurman na kusini mwa Khartoum. Hiyo ikiwa ni jaribio la kuzuia jeshi kutumia silaha nzito na ndege za kivita.

Vita vya Sudan vyatinga mwezi bila matumaini ya kumalizika

Jeshi limekuwa likijaribu kukatisha njia ambazo wanamgambo wanatumia kupata vifaa kutoka nje ya Khartoum. Aidha limekuwa likijaribu kulinda maeneo muhimu ya kimkakati ikiwemo uwanja wa ndege ulioko katikati ya Khartoum na kiwanda cha kusafisha mafuta cha Al-Jaili kilichoko Bahri.

Je makubaliano ya kuweka mtutu chini yataheshimiwa Sudan?

This browser does not support the audio element.

Mapigano hayo yalianza kutokana na mvutano kuhusu mipango ya RSF kutaka kujiunga na jeshi na kushirikishwa kwenye uongozi wa mpito wa kisiasa wa nchi hiyo kuelekea utawala wa kidemokrasia.

Mkuu wa majeshi Jenerali al-Burhan na hasimu wake anayeongoza RSF Jenerali Dagalo maarufu kama Hemedti, walichukua nyadhifa za uongozi kwenye Baraza la kiutawala baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2019, yaliyomuondoa aliyekuwa rais wa muda mrefu wa nchi hiyo na aliyetawala kwa mkono wa chuma Omar al-Bashir.

Miaka miwili baadaye majenerali hao walifanya mapinduzi mengine wakati muda wa kukabidhi utawala kwa raia ulipokaribia. Lakini pande zote mbili zilishindwa kuelewana wakati wapatanishi walikuwa wakijaribu kupiga msasa mpango mpya wa mpito.

(Chanzo: RTRE)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW