1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Milosevic alitoa mshindo kwa mahakama ya The Hague"

Maja Dreyer13 Machi 2006

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanaliangalia tokeo muhimu la mwishoni mwa juma, yaani aliyekuwa rais wa Yugoslavia wa zamani Slobodan Milosevic kufariki dunia katika chumba chake kwenye jela ya Mahakama ya kimataifa mjini The Hague.

Tunaanza na gazeti la “Tageszeitung” kutoka mjini Berlin. Liliandika:
“Kwamba Milosevic alikuwa hakuhukumiwa kabla ya yeye kufariki dunia, kwa kweli ni kosa la mwendeshaji mashtaka mkuu katika mahakamu hayo, Carla del Ponte, licha ya kanusho lake. Kesi ya Milosevic iliendelea kwa miaka minne. Wakati huu wote Milosevic aliweza kutumia mahakama ya The Hague kama jukwaa la kisiasa. Ukiangalia fujo katika kuwaita mashahidi, ni vigumu sana kufahamu mbinu ya upande wa uendeshaji mashtaka.”

Gazeti la “Leipziger Volkszeitung” pia linaweka picha mbaya likiangalia kesi dhidi ya Milosevic. Liliandika:
“Baada ya kazi ngumu ya miaka minne, mahakama ya The Hague na mwendeshaji mashtaka wake mkuu Carla del Ponte anabaki na magofu ya kazi yake. Hukumu haiwezi kutolewa tena. Hivyo, Milosevic alitoa mshindo kwa mahakama hiyo ambayo mwenyewe hakuitambua. Kwa kisheria ,Milosevic anabaki mtu asiye na hatia. Ni kama ndoto mbaya kwa jamii za wahalifu wa mauaji ya Srebenica yanayosemekana kusababishwa na Milosevic.”

Mhariri wa gazeti la “Financial Times Deutschland” lakini anasifu kazi ya mahakama ya The Hague: “Kesi hiyo haikushindwa kwa sababu ilibidi ivunjwe. Kabla yake wengi hawakuamini kuwa inawezekana kuwashika wahalifu wa uhalifu mkubwa kama ule wa nchini Bosnia. Wakati wanafunzi wa historia watakapoangalia kesi hiyo baada ya miaka 10 au 20, jambo muhimu halitakuwa kwamba ilivunjwa lakini kwamba ilikuwepo!”

Na katika gazeti la “Stuttgarter Zeitung” tunasoma maoni yafuatayo:
“Majaji na waendeshaji mashtaka walishindwa kuendesha kesi kwa haraka iliyotakiwa. Hata makubwa zaidi ni mashtaka kuwa mahakama haiwatunza wafungwa kufuata sheria zao. Tayari wafungwa wattu walijiua. Na Milosevic alitafutwa tu saa moja baada ya kifo chake ingawa, kisheria, vyumba vinahitaji kupitiwa kila nusu saa. Taasisi muhimu kama mahakama hiyo haiwezi kufanya makosa haya yanayowawezesha watu wengine kuikosoa.”

Na mwishowe ni uhariri wa gazeti la “Kölner Stadtanzeiger” ulioandika:
“Hata bila ya hukumu dhidi ya Milosevic, bado kesi yake ina umuhimu. Mahakama ya Umoja wa Mataifa ilifanya kazi nzuri kwa ajili ya nchi Yugoslavia ya zamani kwa kumpeleka rais wa zamani kizimbani – jambo ambalo lisingeweza kufikiriwa katika miaka ya tisini. Pamoja na hayo katika kesi 160 za uhalifu wa kivita mahakama ya The Hague ilifichua ukweli wa mambo bila ya kuweza kudanganywa tena. Mahakama haiwezi kufuta uhalifu uliofanywa. Lakini inaweza kufungua njia ya kuelekea kwenye mustakbali ulio na ustaarabu.”

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW