1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mipaka iko wazi Libya

3 Oktoba 2013

Miaka miwili baada ya kuangushwa kwa kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi, nchi hiyo imeendelea kuwa kama pori kaskazini mwa Afrika, huku serikali ikishindwa kudhibiti mipaka.

Wanawake wa Kituareg wakipiga picha maputo katika jangwa la Ghadames mashariki mwa Libya.
Wanawake wa Kituareg wakipiga picha maputo katika jangwa la Ghadames mashariki mwa Libya.Picha: Getty Images

Katika ofisi ya meya wa mji wa Isseyen, muda unaonekana kama vile umesimama. Tangu kumalizika kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi ujao, utulivu umerejea katika ofisi hiyo, na kinachowaleta wageni ofisini hapo kwa sasa ni kupata huduma za intaneti ya setilaiti, ambazo hazipatikani kwingine katika eneo hilo tangu kumalizika kwa mapinduzi.

Lakini kimya hicho kinaongopa. Mji wa Isseyen, ulioko kusini-magharibi mwa mji wa Ghat, ndilo eneo la mwisho kabla ya mpaka wa Algeria na Libya, ambao unatumiwa miongoni mwa mambo mengine, na wasafirishaji wa magendo na pia wapiganaji wa Kituareg kutoka nchini Mali kuingia Libya. Miongoni mwa wapiganaji wanaojipenyeza nchini Libya kupitia mpaka huo, ni pamoja wa wanachama wa kundi la Al-Qaeda katika eneo la Maghreb, AQIM.

Kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Ghadafi.Picha: picture-alliance/ dpa

Hofu ya Al-Qaeda
Hassan Massafer, mwanajeshi kutoka kambi iliyoko mji wa Ubari, kilomita 400 ndani ya Libya, alisema aliwaona wapiganaji wa Al-Qaeda katika eneo hilo, lakini akaongeza kuwa serikali haitaki kujua kuhusiana na hilo. Wakaazi wa eneo hilo wamejawa na hofu, baada ya kuripotiwa kwa msafara wa wapiganaji wa kundi la AQIM waliokuwa na silaha nzito nzito waliokuwa wakielekea upande wa kaskazini.

Lakini baada ya kufuatilia taarifa hizo, iligundulika kuwa msafara huo haukuwa wa wapiganaji wa AQIM, bali walikuwa askari wa kupiga doria. Mkaazi mwingine wa eneo hilo, Abishini Aissa, alisema hofu ya wakaazi wa kusini mwa Libya sio Watuareg na makundi ya Kiislamu, bali magenge ya uhalifu na vurugu kati ya makundi ya kuuza madawa. Aissa anasema katika maeneo ya jangwa mwenye nguvu ndiye anayekula, lakini vijijini hali ni salama kwa sababu watu wanafahamiana.

Lakini kwa ujumla, hakuna anayekataa katika eneo hilo kuwa hali ya usalama ni ya kutisha, na kwamba serikali ya Libya haina udhibiti wa mipaka yake. Meya wa mji wa Ghat, Mohamed Abdelkader, anakiri kuwa mipaka ya eneo hilo iko wazi, na kwamba madawa ya kulevya na silaha vinaingizwa na kutolewa, na kwamba jeshi halina uwezo wa kuwazuwia wala kukabiliana na walanguzi wa dawa za kulevya na makundi yenye itikadi kali.

Pamoja na hayo, meya Abdelkader anasema katika hali halisi, hakuna jeshi nchini Libya. Wakati wa utawala wa Ghadafi, jeshi halikuwa na nguvu kwa sababu kiongozi huyo alikuwa akihofia kupinduliwa, na tangu kuondolewa kwake, mchakato wa kujenga jeshi imara ungali unaendelea. Kwa maeneo ya mpakani, meya Abdelkader anasema hakuna wasimamizi wa kutosha na wakati mwingine wageni wanapita bila pasipoti zao kukaguliwa.

Wanajeshi wa serikali ya Libya.Picha: picture-alliance/dpa

Serikali isiyo na meno
Serikali bado haina mamlaka, kwa sababu licha ya nembo mpya na beji, wapiganaji walioingizwa katika jeshi la serikali wanaendelea kuwa watiifu kwa makamanda wao wanaowasimimamia, na maslahi ya makabila yao na jamii zao kwanza. Kiongozi wa baraza la kijeshi la Murzuk, Kusini-magharibi mwa Libya, Barka Wardougou, anasema namna jeshi lilivyoundwa mara ya kwanza lilikuwa kosa kubwa.

Anasema badala ya uandikishwaji wa kuchagua, serikali ilipaswa kuchagua vijana 12,000 kutoka nchini kote na kuwapeleka kwa ajili ya mafunzo nchini Uingereza, na kisha kuwasambaza kwa kuwachanganya katika maeneo mbalimbali ya nchi, kama njia pekee ya kuunda jeshi lenye ueledi.

Ripoti ya hivi karibuni ya Kamisheni ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa UNCHR na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, ilionyesha kuwa serikali iliacha uongozi wa magereza mikoni mwa makundi ya zamani ya waasi pasipo kuyapa mafunzo yoyote.

Maslahi ya kitaifa, kikabila
Lakini Barka Wardougou hawakilishi tu maslahi ya taifa, bali pia ya kabila lake la Tubu. Kutokana na kuishi mpakani, kabila hilo liligawanywa kati ya mipaka ya Libya na Chad. Sehemu kubwa wako nchini Chad, na kwa wale wachache walioko Libya wanakabiliwa na ubaguzi na chuki kutoka kwa Walibya wengi, ambao wanawaona kama wavamizi hatari. Kanali Wardougou mwenyewe amekuwa akishiriki uasi katika eneo la Sahel, mara zote akiwa upande wa wanaoonewa, kama anavyodai mwenyewe.

Waziri wa mambo ya nje wa Libya, Ashour Shuail.Picha: AFP/Getty Images

Wakati mmoja alikuwa kiongozi wa kile kilichokuwa kikijulikana kama jeshi la ukombozi la Sahel nchini Niger. Kwa mtizamo wake, serikali mjini Tripoli ni kichekesho tu, kwa sababu imewekwa mikononi mwa wapiganaji wenye itikadi kali kutoka mji wa Benghazi.

Anasema serikali hiyo inatuma wapiganaji wa Kiislamu katika maeneo yao ili kuwafanya waamini kuwa ina udhibiti wa maeneo ya mipakani mwa Chad na Niger. Anasema wao ndiyo wanahakikisha utulivu na kuwafuatilia wasafirishaji wa magendo, lakini anakiri kuwa katika mazingira magumu ya jangwa, hata vikosi vyao haviwezi kukaa muda mrefu.

Kukata tamaa kwa watunga sera katika eneo hilo kunaonekana bayana. Mikakati ya usalama, ambayo inazungumziwa sana mjini Tripoli, kusini mwa Libya haiendi mbali zaidi ya kuandikwa tu kwenye makaratasi.

Mwandishi: Stocker, Valerie
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Josephat Nyiro Charo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW