Mipango mitatu kwa Afrika lakini haina uwiano
5 Mei 2017Waziri wa uchumi wa Ujerumani Brigitte Zypries anahudhuria kongamano la kiuchumi duniani kuhusu Afrika (World Economic Forum Afrika) mjini Durban, Afrika Kusini. Waziri Zypries ameandamana na ujumbe wa wawakilishi wa biashara wa Ujerumani. Wafanya biashara hao kutoka Ujerumani wanadhamiria kujikita katika miradi mikubwa ya ujenzi barani Afrika
"Pro Africa - Ufanisi kwa Afrika” ndio mpango kazi wa waziri huyo wa uchumi wa Ujerumani. Ni mpango unaokusudia kufungua fursa zaidi kutoka katika sekta binafsi barani Afrika, ili kuleta uwezekano wa upatikanaji wa ajira katika nchi hizo na hivyo kukabiliana na wimbi la uhamiaji linalokuja barani Ulaya.
Katika mwaka huu ambapo Ujerumani ndio rais wa kundi la G20 na katika hali ya kukabiliwa na wimbi la wakimbizi ajenda inayopewa umuhimu zaidi ni ya bara la Afrika. Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgand Schaeuble amesema katika wizara yake inadhihirika jinsi gani kulivyo na ushindani kati ya idara mbalimbali zinazoshindana kuwasilisha mawazo bora kwa ajili ya Afrika na amesema kwamba anafikiri hilo ni jambo zuri. Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble anaunadi mpango wake wa huduma kwa Afrika ni mpango unaolenga kuboresha hali ya uwekezaji endelevu kutoka kwa wawekezaji binafsi ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwekezaji katika miundombinu na vilevile kubuni ajira. Mpango huu utahimiza uwekezaji wa pamoja baina ya nchi za Afrika zitakazokuwa na nia ya kujiendeleza pamoja na mashirika ya kimataifa na nchi washirika.
Lakini Nachalila Nkumbo mkurugenzi mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Afrika linaloitwa ONE ana wasiwasi kwamba kumekuwa hakuna mkakati wa jumla wa serikali ya Ujerumani amesema kuwa na wawekezaji zaidi kutoka Ujerumani ni jambo zuri lakini bado kuna watu ambao wanaishi katika hali ya umasikini mkubwa barani Afrika. Watu hao wanahitaji msaada mkubwa kutoka serikalini au misaada kutoka kwa wafadhili kwa hivyo uwekezaji binafsi unahitajika lakini lazima uandamane na misaada pamoja na michango mikubwa kutoka kwenye serikali za Afrika.
Huku swala la kuwa na ushirikiano na nani likiwa halipewi kipaumbele wawakilishi wa kampuni ya Siemens na kampuni ya nishati ya nchini Sudan walitia saini makubaliano ya sehemu ya "Pro Afrika", mbele ya Waziri wa uchumi wa Ujerumani Brigitte Zypries akiwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Siemens Joe Kaeser.
Mwandishi: Zainab Aziz/ Hilke Fischer/ LINK: http://www.dw.com/a-38705756
Mhariri: Iddi Ssesanga