1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Miripuko ya mabomu imerindima tena mjini Khartoum

23 Mei 2023

Matumaini ya kuheshimiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Marekani na Saudi Arabia mjini Jeddah yameyumba kufuatia mashambulizi hayo.

Sudan Konflikte Kämpfe
Picha: AFP

Makombora yalisikika katika sehemu kadhaa mjini Khartoum, huku ndege za kivita zikionekana katika anga za mji huo, na kuongeza hofu kwamba mapigano makali huenda yakazuka muda wowote na kuondoa matumaini ya wasudan yaliyojitokeza baada ya pande mbili kuridhia kusitisha mapigano kwa wiki moja.

Atef Salah El-Din, mkaazi wa Khartoum, aliye na miaka 42 amesema matumaini yake makubwa yalikuwa ni kuheshimiwa na kufanikishwa kwa makubaliano hayo ili maisha yarejee kama kawaida, wawe huru na kurejea kazini.

Baada ya mapigano makali kati ya pande mbili za kijeshi zinazohasimiana, ikiwa ni upande wa kiongozi wa jeshi nchini humo, Abdel Fattah al Burhan na kiongozi wa kikosi cha wanamgambo wa RSF Mohammed Hamdan Dagalo walikubaliana siku ya Jumamosi kusitisha mapigano kwa siku saba ili kuridhia misaada ya kiutu kufika katika eneo la mzozo.

Lakini kufuatia ripoti za milio ya miripuko mjini Khartoum, Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken ametoa onyo kali kwa majenerali wa pande hizo mbili kupitia ukurasa wake wa twitter kwamba, waheshimu makubaliano yaliyotiwa saini hivi karibuni au wakabiliwe na uwezekano wa kuwekewa vikwazo.

Shinikizo la Marekani

Picha: AFP/Getty Images

Blinken amesema waliongoza juhudi za kupatikana kwa makubaliano hayo, lakini jukumu la kuyafanikisha linabakia kuwa la jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF. Mwanadiplomasia huyo ametoa tahadhari hiyo wakati Marekani ikitangaza kutoa msaada wa kitita cha dola milioni 245 kuisaidia Sudan na nchi jirani kukabiliana na mzozo wa kipinadamu uliozushwa na mapigano yanayoendelea. 

Wakati uo huo, wanaharakati wameuandikia ujumbe wa Umoja wa Mataifa, wakilalamika kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu dhidi ya raia wa taifa hilo uliotokea wakati vita vilipopamba moto. Hadi sasa vita hivyo vimesababisha watu milioni 1.1 kupoteza makaazi yao wakiwemo watu zaidi ya 250,000 waliokimbilia nchi jirani kama Ethiopia na Sudan Kusini.

Huku hayo yakiarifiwa maafisa wa shirika la msalaba mwekundu wamesema wakimbizi wa Sudan wanaendelea kumiminika nchini Chad kwa wingi na itakuwa ngumu kuwapa wote makaazi salama kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua mwishoni mwa mwezi Juni.

Shirika hilo limesema wakimbizi 60,000-90,000 wameingia nchini Chad kufuatia mzozo huo unaendelea wa Sudan. Asilimia 80 ya wale wanaowasili nchini humo ni wanawake na watoto.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wakimbizi UNHCR limesema lina mipango ya kuwaondoa wakimbizi walioko katika maeneo ya mipakani na kuwapeleka katika makambi yalioko nchini Chad pamoja na kufanya juhudi ya kufungua makambi mengine matano. Msemaji wa shirika hilo nchini Chad Eujin Byun amesema wakimbizi wengi wamewapoteza jamaa zao na nyumba zao kuchomwa moto.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW