1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misaada ya dharura ya Marekani imekwama mpakani Venezuela

Sekione Kitojo
8 Februari 2019

Malori yaliyobeba misaada ya kiutu  kwenda Venezuela yamewasili katika mpaka wa Colombia, ambako viongozi wa upinzani wameapa  kuingiza katika chini hiyo yenye matatizo licha ya upinzani kutoka kwa rais Nicolas Maduro.

Venezuela Grenzübergang zu Kolumbien Tienditas Brücke bei Cucuta
Picha: Getty Images/AFP/E. Estupinan

Malori  mawili  yaliyojaa  chakula  cha  msaada  na  madawa yaliwasili  katika  mpaka  wa  Colombia  katika  mji  wa  Cucuta, ambao  uko upande  wa  pili  wa  mto  kutoka  Venezuela.

Malori ya misaada ya kiutu iliyokwama katika mkapa wa Colombia na VenezuelaPicha: picture-alliance/AP/F. Vergara

"Marekani inaleta  bidhaa, ikiwa  ni  pamoja  na  chakula, vyakula vya  ziada  vya virutubishi  mwilini, bidhaa za  usafi pamoja na madawa, nchini  Colombia ili viweze  kuwafikia  wale  wenye  uhitaji nchini  Venezuela , haraka  iwezekanavyo,"  amesema  afisa  wa Marekani , akizungumza  kwa  masharti  ya  kutotajwa  jina kwasababu  hana  mamlaka  ya  kulizungumzia  suala  hilo.

Mtazamo  wa  mvutano wa  kisiasa nchini  Venezuela  sasa unatuwama  katika  hali  iwapo  Maduro ataruhusu  msaada  huo kuingia  nchini  humo, hatua  ambayo  inatarajiwa  katika  siku  zijazo.

Maduro  anakataa  kwamba  kuna  mzozo  wa  kiutu  nchini  humo  na kusema  Venezuela  sio  nchi  ya  omba  omba. Jeshi  la  Venezuela limeweka  vizuwizi  katika  daraja  linalounganisha  nchi  hizo  mbili kwa  makontena  katika  juhudi  za kujaribu  kuzuwia  misaada  hiyo kuingia  nchini  humo.

kiongozi  wa  upinzani  Juan Guaido , ambaye  anaimba  jumuiya  ya kimataifa  kutoa  msaada, amesema  ni  muhimu  katika  nchi  hiyo inayokabiliwa  na  upungufu  wa  chakula  na  madawa.

Rais Nicolas Maduro alipoapishwa kuwa rais baada ya uchaguzi wa hapo 2018Picha: picture-alliance/AP/A. Cubillos

Urusi  na  China zamuunga  mkono Maduro

Guaido , ambaye anaungwa  mkono  na  mataifa  40, ikiwa  ni pamoja  na  Marekani, anataka  kumuondoa  madarakani  Maduro kufuatia  uchaguzi  wa  mwaka  2018  ambao  mataifa  mengi yameshutumu  kuwa  ulikuwa  wa  udanganyifu. Washirika  wa  muda mrefu  Urusi  na  China  pamoja  na  mataifa  mengine  kadhaa yanaendelea  kumuunga  mkono  Maduro.

Kiasi  ya  wanaharakati  wapatao  12 wa  haki  za  binadamu walisimama  katika  lango la  kuingilia  katika  daraja  la  kimataifa  la Tienditas  katika  upande  wa  Colombia, wakidai  Maduro  aruhusu msaada  huo  wa  dharura  kuingia  nchini  Venezuela. Walipunga bendera  wakati  magari  ya polisi  wa Colombia yaliyowabeba  polisi waliokuwa  na  silaha  na  maafisa  wengine  yakipita  siku  nzima. Luis Escobar, raia  wa  Venezuela  ambaye  anaishi  nchini Colombia  baada  ya  kukimbia  taifa  lake  lililokumbwa  na  matatizo, amesema  mke  wake  ana  kansa ya  ziwa ambayo  imefika  katika hatua  ya  juu  na  kumtaka  Maduro kukubali msaada.

Akitokwa  na  machozi , alielezea  vipi  mkewe alishindwa  kupata matibabu  nchini  Venezuela  na  kwamba  katika  wakati  walipopata kumuona  daktari  nchini  Colombia, ugonjwa  wake ilikuwa  tayari umetapakaa  mno.

Mji wa mpakani wa Cucuta , kuelekea Venezuela kutoka ColombiaPicha: DW/T. Käufer

"Niko  hapa  kwasababu , kwa  bahati  mbaya, mke  wangu  anakufa, " Escobar  alisema.

"Lakini  leo  niko  hapa  kwa  ajili  ya  Wavenezuela  ambao wanataabika  kama  mke  wangu. Dunia inapaswa  kufahamu  juu  ya hili."

Kanali wa zamani aungama

Wakati  huo  huo , waziri  wa  mawasiliano  wa  Venezuela , Jorge Rodriguez , alijitokeza  katika  televisheni  akidai  kwamba  idara  ya ujasusi  ya  Colombia , CIA  na mbunge wa  upinzani   wa  Venezuela ambaye  anaishi  uhamishoni  Julio Borges wanahusika  na  mpango wa  kumpindua  Maduro.

Waandamanaji wakiandamana mjini Madrid kuunga mkono rais aliyejitangaza nchini Venezuela Juan GuaidoPicha: picture-alliance/NurPhoto/O. Gonzalez

"Muuaji  kama  Borges  ni  lazima  aweke  kando  unafiki," Rodriguez alisema. "hakuna  demokrasia , hakuna msaada  wa  kiutu. Kitu  gani atasema, hivi  sasa  ambapo washirika  wake  wamemuumbua?

Rodroguez  alionesha  video  ya  kile  alichosema  kuwa  ni kuungama  kwa  kanali  mstaafu  kutoka  katika  kikosi  cha jeshi  la ulinzi  la  taifa  Oswald Garcia Palomo  kuwa  ni  ushahidi  wa  madai hayo  ya  njama  ya  mapinduzi. Mkosoaji  mkubwa  wa Maduro, Palomo  amezungumzia  wazi kuhusu  kukusanya  wanajeshi  nje  ya nchi  kumuondoa  kiongozi  wa  Venezuela  kutoka  madarakani. Alikamatwa  mwezi  uliopita baada  ya  kuingia  nchini  Venezuela kwa  siri akitokea  Colombia.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape

Mhariri : Yusuf,  Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW