1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misaada ya Fedha kuhimiza Ulinzi wa Misitu

17 Desemba 2009

Misitu inatoweka kwa kasi kubwa kote duniani. Miti inapokatwa hata mazingira ya wanyama na mimea ya aina mbali mbali huteketezwa na vile vile huchangia kuzidisha hali ya joto duniani.

A car is seen on a road that crosses the dense Amazon rainforest near the northern city of Manaus, Brazil, Friday, Sept. 21, 2007. New studies suggest the Amazon may be approaching a tipping point, at which the drier conditions caused by deforestation will reduce rainfall enough to transform the humid tropical forest into a giant savanna. (AP Photo/Andre Penner)
Msitu wa Amazon karibu na mji wa Manuas kaskazini ya Brazil.Picha: AP

Kwa hivyo inashangaza sana kuwa mpaka sasa, misitu haikupewa umuhimu mkubwa hivyo katika makubaliano ya mazingira ya Umoja wa Mataifa. Misitu inateketezwa kwa sababu mbali mbali. Kwa mfano nchini Brazil misitu ya asili inakatwa ili kupata nafasi ya kufuga ng'ombe: barani Afrika na Indonesia miti yenye thamani inateketezwa ili kuwa na mashamba ya michikichi. Misitu iliyotoweka imechangia kuongeza hali ya joto duniani kwa hadi asilimia ishirini - hiyo ni zaidi ya moshi unaotolewa na magari, meli na ndege zote kwa jumla kote duniani.

Kwa hivyo, katika mkutano wa hali ya hewa mjini Copenhagen misitu inapewa kipaumbele katika mpango maalum - maarufu kwa ufupi REDD. Azma ya mpango huo ni kupunguza viwango vya gesi inayotoka misituni, miti inapopunguzwa au inapoteketezwa kabisa kwa moto. Kuambatana na mpango huo mpya, wamiliki misitu katika siku zijazo watalipwa fedha ikiwa hawatoikata miti yao na hivyo kusaidia kuhifadhi mazingira. Tatizo hadi sasa ni kuwa kanuni za Itifaki ya Kyoto, hazitumiwi kulinda misitu na kuhimiza ulinzi wa mazingira. Ulinzi wa misitu haukupata kipaumbele katika mkataba wa kuhifadhi mazingira.

Lakini safari hii katika mkutano wa Copenhagen, ulinzi wa misitu unatazamiwa kufungamanishwa na mkataba wa hali ya hewa. Hata hivyo, bado kuna masuala mengi ya kujadiliwa. Mpango huo mpya hasa ni muhimu kwa Indonesia na Brazil kwani nchi hizo ni miongoni mwa wachafuzi wakuu watano wa mazingira duniani. Moshi unaosababishwa na Brazil na Indonesia kila mwaka na kuchafua hali ya hewa kwa sababu ya misitu inayoteketezwa, ni zaidi ya ule unaotoka nchi zote za Afrika kwa jumla na kuchafua mazingira. Kwa hivyo Waziri wa Mazingira wa Brazil Carlos Minc anaeshiriki katika mkutano wa Copenhagen amesema:

"Brazil inaunga mkono mpango wa REDD kama mfumo wa ziada unaoweza kutumiwa badala ya viwango vya kupunguza moshi."

Lakini ameongezea kuwa hiyo isimaanishe kuwa nchi tajiri hazitowajibika.Brazil ina hofu kuwa misitu ikihifadhiwa katika nchi hizo za kusini,basi nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda huenda zikatumia viwango hivyo ili zisiwajibike kupunguza utoaji wa moshi unaochafua hali ya hewa.

Ili mkutano wa Copenhagen uweze kufanikiwa katika ulinzi wa misitu, masuali mengi yaliyokuwepo yanapaswa kupatiwa ufumbuzi katika mpango wa REDD.

Mwandishi:Beck,Johannes/ZPR/P.Martin

Mhariri: M.Abdulrahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW