Misaada ya fedha kwa Hamas
18 Aprili 2006Baada ya Marekani na Umoja wa Ulaya kuunyima utawala wa Palestina wa chama cha Hamas msaada wa fedha ,Urusi kwa muujibu wa ripoti ya gazeti moja- imejitolea kuusaidia utawala huo kwa kima cha dala milioni 10.
Fedha hizo zitatumika kuhudumia miradi ya kibinadamu.Na vipi nchi nyengine za kiislamu zinausaidia utawala wa Hamas ?
Serikali ya chama cha HAMAS ilipoingia madarakani, ilikuta hazina tupu ilioachiwa na utawala uliopita.
Isitoshe,ulijikuta umerithi madeni ya hadi dala bilioni 1.5.Na hakuna matumaini ya hazina yao kutengenea.Kwani, kama kupiga msumari juu ya donda, Umoja wa Ulaya na Marekani ziliamua kuzuwia msaada wao wa fedha katika mfuko wa hazina ya wapalestina.
Kwa mwaka uliopita wa 2005 kima kilikua kiasi cha dala milioni 240 kutoka Marekani na dala milioni 280 kutoka UU.
Israel nayo ikazuwia kutoa dala milioni 50 ilizokusanya kama ushuru na kodi kwa niaba ya utawala wa ndani wa wapalestina.
Serikali ya wapalestina kikawaida huhitaji si chini ya dala milioni 170 kila mwezi ili kukidhi mahitaji ya mishahara ya watumishi wake 140.000.Hawa pekee wanahitaji dala milioni 115.
Kwa hali hii, wafadhili wengine waliojitolea kuwaokoa wapalestina, msaada wao si mkubwa hivyo:mawaziri wa nje wa Jumuiya ya nchi za kiarabu waliafikiana wakati wa kikao chao cha Khartoum hivi majuzi kuwasaidia wapalestina kwa kima cha dala milioni 50 kwa mwezi.Dala milioni 50 zaidi zimeahidiwa kutolewa na Iran na ikatoa pengine hata dala milioni 100.
Waziri wa nje wa palestina ,Mahmoud Al-Azhar,anajaribu wakati huu kuzuru nchi kadhaa za kiarabu kuomba msaada zaidi wa fedha ,lakini serikali za huko zinaitikia shingo upande.
Waziri wa nje wa Syria Farouk A-Shara, ingawa ametoa mwito kusaidiwa wapalestina,hakufika mbali zaidi ya kuchangisha fedha kutoka kwa wananchi wa syria.
Nchini Jordan, akiba ya kuwachangia wapalestina katika Arab Bank ilidumu siku chache tu,kwani haukupita muda A/C hiyo ilifungwa na serikali.
Inadhaniwa Marekani iliitia shindo kubwa serikali ya Jordan kuifunga A/c hiyo.
Hivi sasa kuna akiba moja tu ya kuchangia katika Banki ya Misri mjini Kairo.Mabanki kadhaa ya saudi Arabia yamekataa kukusanya michango kwa serikali ya hamas,kwani yanahofia vikwazo vya Marekani.Hata katika nchi za Ghuba zinazotoa mafuta hali ni sawa na hiyo.
Hali ni hiyo ingawa nchi za kiarabu na za Ghuba zingeweza nazo kuishinikiza Marekani kwavile zina raslimali kubwa ya fedha za dala kutoka nishati ya mafuta .
Hatahivyo, juhudi zote hizo hazitazuwia koo za kitajiri na watu binafsi kukichangia chama cha MAMAS.Kwa upande mmoja,ni kutokana na kukihurumia chama hicho cha kiislamu na kwa upande mwengine kama kinga dhidi ya vikundi vyenye itikadi kali ya kiislamu.
Kama ilivyojionea zamani chama cha Ukombozi wa wapalestina (PLO) chama cha HAMAS kitabidi kutambua nacho kwamba ahadi za kukisaidia kifedha ni ni swali moja na kutolewa hasa fedha ni swali jengine.