1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misaada ya kibinadamu yaanza kuwasili Tonga

20 Januari 2022

Ndege za kwanza kupeleka misaada ya kibinadamu zimewasili nchini Tonga, siku tano baada ya nchi hiyo kukumbwa na mlipuko wa volkano na mvua kubwa zilizoiathiri jamii na kuchafua sehemu kubwa ya maji ya kunywa.

Neuseeland | Hilfsgüter für Tonga
Picha: CPL Dillon Anderson/New Zealand Defence Force/AP/picture alliance

 

Ndege mbili kubwa za kijeshi kutoka Australia na New Zealand zimewasili katika uwanja mkuu wa ndege wa Tonga ambao hivi  majuzi tu ulisafishwa safu nene za majivu baada ya juhudi kubwa.

Waziri wa maendeleo ya kimataifa na pasifiki wa Australia Zed Seselja, alipongeza kuwasili kwa ndege ya taifa hilo aina ya C-17 na kusema imebeba bidhaa zinazohitajika zaidi za msaada wa kibinadamu akiongeza kwamba ndege nyingine ya C-17 iko njiani kulekea katika eneo hilo. Miongoni mwa vifaa vilivyoletwa na ndege hiyo inasemekana kuwa kifaa cha kupakua kilicho na fagio kusaidia kuondoa majivu katika njia ya kuruka ndege.

New Zealand yathibitisha kuwasili kwa ndege

New Zealand pia imethibitisha kuwa ndege yake aina ya C-130 Hercules pia imetua. Waziri wa mambo ya nje wa New Zealand Nanaia Mahuta amesema kuwa ndege hiyo imebeba bidhaa za misaada ya kibinadamu na majanga, ikiwa ni pamoja na vyombo vya maji, vifaa vya makazi ya muda, jenereta, vifaa vya usafi na vya matumizi ya familia pamoja na vifaa vya mawasiliano.

Mlipuko wa volkano ya chini ya maji uliotokea Hunga Tonga-Hunga Ha'apaiPicha: Tonga Geological Services/REUTERS

Lakini vizuizi vikali vya kuthibiti kuenea kwa virusi vya corona ambavyo vimelisaidia taifa la Tonga kutokuwa na visa vya maambukizo, vinaashiria kuwa uwasilishaji wa bidhaa hizo za msaada hautahusisha mgusano. Kamanda wa jeshi wa New Zealand James Gilmour, amesema hakutakuwa na ukaribu kati ya jeshi la nchi yake na mtu yeyote katika eneo hilo na kwamba wanajeshi hao wanatarajiwa kukamilisha zoezi hilo katika muda wa dakika tisini.

Mawasiliano ya simu kati ya taifa hilo na maeneo mengine ya dunia pia yaliunganishwa tena jana jioni ijapokuwa kurejesha huduma kamili ya mtandao inauwezekano wa kuchukuwa mwezi mmoja ama zaidi.

Maji safi ya kunywa ndilo suala la dharura 

Akizungumza na shirika la reuters kutoka mji mkuu Nuku'alofa, mwanahabari Marian Kupu, amesema raia wa Tonga wanasafisha vumbi lote lililosababishwa na mlipuko huo wa volkano lakini wanahofu kuwa huenda wakaishiwa na maji ya kunywa. Kupu amesema kuwa kila nyumba ina matangi yake ya maji lakini mengi yamejazwa vumbi na kuyafanya kutokuwa salama kwa kunywa.

Umoja wa Mataifa umesema kuwa takriban watu elfu 84 hii ikiwa zaidi ya asilimia 80 ya idadi jumla ya watu nchini humo wameathirika vibaya kutokana na janga hilo huku suala la maji safi ya kunywa likiwa la dharura kwasasa katika uokoaji wa maisha.

 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW