1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misaada ya kiutu kwenye Pakistan

Richard Madete12 Oktoba 2005

Harakati za misaada kwa wahanga wa tetemeko la ardhi kwenye eneo la Kashmir – upande wa Pakistan, imeanza kuwa na mafanikio zaidi hii leo baada ya helikopta za Marekani na Ujerumani kuwasili. Hata hivyo maelfu ya wahanga wa tetemeko hili bado hawajapata msaada wowote, siku tano baada ya tetemeko lenyewe kutokea hapo Jumamosi iliyopita.

Harakati za kuwasaidia wahanga wa tetemeko la ardhi
Harakati za kuwasaidia wahanga wa tetemeko la ardhiPicha: AP

Mashirika ya kimataifa ya misaada ya kiutu kutoka nchi mbalimbali yanajitahidi jinsi yawezavyo kuyafikia maeneo ya mbali yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi huko kusini mwa Asia. Mpaka hivi karibuni baadhi ya wahanga wa tetemeko la ardhi lililotokea Jumamosi tarehe 8-Oktoba, walikuwa hawajapata misaada muhimu ya chakula, malazi na tiba.

Hali ni mbaya zaidi kwenye mji wa MUZAFFARABAD ulio kwenye upande wa Pakistan katika eneo la KASHMIR. Wahusika wanahofia maiti nyingine kuwa zimezikwa kwenye magofu ya nyumba zilizobomolewa na tetemeko hilo.

Inatia moyo sasa kuona kuwa, hata kwenye eneo hilo misaada ya kiutu imeanza kuingia, hususani baada ya helikopta za Marekani na Ujerumani kuanza kusambaza misaada hii.

Tangu masaa 24 yaliyopita, helikopta 95 zinapeleka misaada ya kiutu katika maeneo mbalimbali yaliyoathirika.

Msemaji wa jeshi la Pakistan, Meja FAROOG NASIR, amenukuliwa akisema, baada ya mvua kusita, misaada ya chakula na dawa inaweza sasa kupelekwa kwenye maeneo hayo kwa njia ya anga, na hapohapo kuwasafirisha majeruhi kwenye vituo vya afya.

Mji mkuu wa eneo la Pakistani huko Kashmir, MUZAFFARABAD, ulikumbwa na tetemeko kubwa la ardhi la kiwango cha Richter Scale 7.6 hapo Jumamosi iliyopita na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 23,000 nchini Pakistani na kuwaacha watu milioni 2.5 bila makazi.

Haya ni maafa makubwa kabisa kwa Pakistani katika historia yake. Viongozi wa nchi wana wasiwasi kwamba, idadi ya wahanga inaweza kuongezeka katika siku zijazo, baada ya kusafisha magofu ya nyumba zilizobomolewa na kugundua maiti nyingine kwenye maeneo hayo. Maeneo mengi ya miji na vijiji huko kaskazini mwa Pakistani yanatumiwa sasa kwa mahema ya maelfu ya wakimbizi ambao wanangojea misaada.

Wengi wao wanalalamika vikali kwa nini misaada hii imechelewa. Hali hii imesababisha baadhi ya wakimbizi hao kuanza kuvamia magari ya misaada.

Hata hivyo Wafanyakazi wa shirika la msalaba mwekundu wamesema, wanaelewa hali ngumu inayowasibu wahanga wa tetemeko la ardhi. Msemaji wa shirika hili, Bi. Layla BERLEMONT, amenukuliwa akisema: “Mtu aliyekumbwa na maafa, hawezi kuelewa kwa nini hapewi msaada haraka iwezekanavyo, hasa pale anapoona ndugu zake wanakufa. Hasira na kukata tamaa ni jambo la kawaida. Hata hivyo lazima waelewe, tatizo siyo kutokuwa na nia ya kuwasaidia, bali ni vikwazo asilia, kama vile mvua na mmommonyoko wa udongo unaoziba barabara na hivyo kukwamisha magari yanayopeleka misaada.”

Mratibu wa misaada ya kiutu ya Umoja wa Mataifa, JAN EGELAND, amekwenda Pakistan hii leo, baada ya kuahirisha ziara yake kwenye eneo lililokumbwa na maafa ya Tsunami huko Indonesia. Kiongozi huyu amewasifu wafanyakazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kufanikisha misaada ya kiutu muda mfupi tu baada ya tetemeko hilo kutokea.

Naye waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condooleza Rice amewasili Pakistan hii leo, baada ya kufupisha ziara yake ya Afghanistan. Akiwa nchini Pakistani anatarajiwa kukutana pia na kiongozi wa nchi PERVES MUSHARRAF.