1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misaada yaanza kuwasili Ufilipino

15 Novemba 2013

Idadi ya watu waliofariki Ufilipino kutokana na kimbunga Haiyan imeongezeka mara dufu, na kufikia 4,000, wakati helikopta za jeshi la Marekani na meli zimeanza kupeleka misaada na madaktari katika eneo la maafa.

TACLOBAN, PHILLIPINES - NOVEMBER 14: In this handout provided by the U.S. Navy, hospital Corpsman 3rd Class Eric Chiarito (L) of Hyde Park, N.Y., and Marine Sgt. Jonathan Thornton, of Lake Havasu, Arizonia, load supplies onto a forklift at Tacloban Air Base in support of Operation Damayan November 14, 2013 in Tacloban, the Phillipines. The George Washington Carrier Strike Group and the 3rd Marine Expeditionary Brigade are assisting the Philippine government in response to the aftermath of Typhoon Haiyan (Yolanda). (Photo by Ricardo R. Guzman/U.S. Navy via Getty Images)
Misaada ya kimataifa inayopelekwa TaclobanPicha: Getty Images

Katika mji wa Merida uliopo kisiwani Leyte , taka bado zimezagaa barabarani kutokana na mabaki ya majengo yaliyoporomoka.

Kimbunga Haiyan kimeshambulia mno katika eneo hilo. Takriban wiki moja baada ya kimbunga hicho wakaazi wa mji wa Merida wameanza kazi ya ujenzi mpya na baadhi ya nyumba zimeanza kutumika. Mvua bado inaendelea kunyesha na wakaazi wa mji huo hujikusanya pamoja katika nyumba ambazo zimebakia na paa juu yake na zile ambazo zimeanza kujengwa na wanajihifadhi kwa pamoja.

Juhudi za kuwasaidia watu walionusurika na kimbunga Haiyan nchini Ufilipino zimeongezeka kuanzia leo, licha ya kuwa serikali imekiri kuwa kasi yale bado ni ndogo.

Helikopta za jeshi la Marekani zikipeleka misaada UfilipinoPicha: Getty Images

Waziri wa mambo ya ndani Mar Roxas amesema kuwa katika mji wa Tacloban , mji mkuu wa jimbo lililoathirika kwa kiasi kikubwa la Leyte, malori yaliyobeba mahitaji mbali mbali yamefika katika miji 30 kati ya 40 katika jimbo hilo.

Usafishaji waanza

Wafanyakazi wakiwa na misumeno ya umeme wamekuwa wakikata miti iliyoanguka mjini Tacloban wakati malori yakibeba miili ya watu waliofariki pamoja na taka zilizozagaa mitaani, na wengine wakikarabati nyumba zilizoporomoka.

Rais Benigno Aquino, ameshindwa kutambua ukubwa wa maafa hayo, na amekosolewa kutokana na kasi ndogo ya usambazaji wa misaada pamoja na makadirio yenye utata ya watu waliofariki, hususan katika mji wa Tacloban, mji ambao umeathirika mno na kimbunga hicho.

Rais wa Ufilipino Benigno S. Aquino akiwafariji wahanga wa maafa ya kimbunga HaiyanPicha: picture-alliance/dpa

Meya aomba radhi

Taarifa katika jengo la halmashauri ya mji wa Tacloban imekadiria kuwa watu 4,000 wamefariki , ikiwa ni ongezeko kutoka idadi ya watu 2,000 waliotangazwa siku moja kabla katika mji huo pekee. Hata hivyo meya wa Tacloban Alfred Romualdez aliomba radhi na kusema kuwa idadi hiyo ni kwa eneo lote la kati la Ufilipino.

Waziri wa mambo ya ndani Mar Roxas amesema kuwa juhudi za kutoa misaada zinaendelea, licha ya kuwa kasi yake ni ndogo bado. Amesema kuwa kila siku inakuwa bora zaidi kuliko siku iliyopita. Haiwezekani kasi kuwa kubwa katika hali kama hii kwasababu watu wengi mno wameathirika na miundo mbinu imeharibika.

Sandra Bulling kutoka katika shirika la kutoa misaada la Care International amesema misaada imeanza kuwafikia walengwa.

"Kwa hivi sasa misaada yetu ya chakula imo njiani kutoka Manila kuja hapa kisiwani. Misaada hiyo itawasili kesho na tutaweza haraka iwezekanavyo kugawa misaada katika eneo la Mormoc. Na mpango ni kwamba katika muda wa siku chache zijazo tutaweza kutumia fursa hii, kufikisha misaada hiyo Merida ama Isabel. Na katika siku chache zijazo tutaleta vifaa vya ujenzi, ili watu waweze kupata mahali pa kuishi."

Bado mvua inanyesha na hakuna mahali pa kujihifadhiPicha: Reuters

Lakini wakati juhudi za kutoa misaada zikiendelea , wataalamu kutoka shirika la afya ulimwenguni WHO pamoja na mashirika mengine yamerudia ushauri wao kuwa serikali ya Ufilipino inapaswa kulenga juhudi zake za kutoa misaada kwa watu walionusurika, badala ya kushughulikia waliofariki.

Mwandishi: Peter Hille / ZR / Sekione Kitojo

Mhariri: Daniel Gakuba

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW