1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mishahara ya wachezaji yapunguzwa kutokana na COVID-19

23 Machi 2020

Ligi kubwa kabisa za kandanda barani Ulaya bado zimesitishwa na wachezaji wanaendelea kukumbwa na shinikizo la kupunguzwa mishahara yao.

Coronavirus - Köln
Picha: picture-alliance/dpa/F. Gambarini

Wakati mwingine, ni kwa hiari kama vile Borussia Moenchengladbach wanaowania ubingwa wa Bundesliga msimu huu, ambapo wachezaji walitoa ofa kwa klabu hiyo kupunguzwa mishahara yao.

Wakati mwingine, wachezaji hawana namna. Nchini Scotland, klabu ya Hearts imewaomba wachezaji wake wote na wafanyakazi kukubali punguzo la asilimia 50 la mishahara yao, au mikataba yao isitishwe.

Kupunguzwa mishahara kunafanyika wakati vilabu kote Ulaya vikipambana  na uhaba wa ghafla wa fedha. Mishahara ya msimu ilifanywa kwenye bajeti ya matarajio ya mapato kutoka kwenye ada za matangazo ya televisheni, ufadhili na mauzo ya tiketi, ambayo yote yamepungwa au kutoweka kabisa.

Ni kutokana na hali hii ya kifedha ambapo makamu wa rais wa shirikisho la kandanda Ujerumani – DFB Rainer Koch amesema mechi za ligi kuu ya kandanda Ujerumani – Bundesliga bila mashabiki uwanjani huenda zikahitajika ili kuvisaidia vilabu na wengine katika biashara hiyo punde tu michezo itaanza kutimua vumbi tena kutokana na janga la virusi vya corona.

Kama tu nchi nyingine, Ujerumani inalenga kuukamilisha msimu wa ligi kwa sababu mashindano ya Euro 2020 sasa yameahirishwa kwa mwaka mmoja. Kama msimu utafutwa kabisa, vilabu vinaweza kupoteza euro milioni 750 na Koch ametoa wito wa kuchezwa mechi bila mashabiki viwanjani ili kuepusha hali ya aina hiyo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW