Misimamo tofauti kuhusu wahamiaji Ujerumani
27 Desemba 2017Haya yanajiri wakati ambapo vyama hivyo vinajitayarisha kwa mazungumzo ya kuunda serikali mwakani. Tofauti hiyo inatatiza mazungumzo hayo.
Uamuzi wa Kansela Angela Merkel mwaka 2015 wa kuwakubalia zaidi ya wahamiaji milioni moja kuingia Ujerumani, wengi wakiwa wanatoroka mapigano Mashariki ya Kati, ni jambo lililobadilisha sura ya Ujerumani katika suala la idadi ya watu na hatua hiyo ilivipa motisha vyama vya mrengo wa kulia na ikasababisha na matokeo mabaya katika chama chake na kile cha SPD katika uchaguzi wa Septemba.
Katika mahojiano naibu kiongozi wa chama cha CDU Thomas Strobl na Waziri wa Mambo ya nje ya Ujerumani Sigmar Gabriel, walielezea njia za kuwavutia tena wafuasi wao wasioridhika na hali ilivyo.
Gabriel anataka serikali za majimbo zipewe fidia kwa kuwapa hifadhi wakimbizi
Strobl aliliambia gazeti la Heilbronner Stimme kwamba Ujerumani inastahili kuweka kiwango cha wahamiaji wanaoingia nchini humu kuwa 65,000 kwa mwaka kinyume na kile kiwango cha wahamiaji 200,000 kilichokuwa kinapendekezwa na Wahafidhina.
Lakini Gabriel ambaye chama chake cha SDP huenda kisikubali kiwango hicho, amependekeza kwamba serikali za majimbo hapa Ujerumani na kote Ulaya zitapewa fidia iwapo zitakubali kuwapa hifadhi wakimbizi.
Gabriel ameliambia gazeti la Funke na hapa namnukuu, "ikifanyika hivyo, serikali hizo zitaamua zenyewe ni wakimbizi wangapi zinazowataka, hilo litaiondoa dhana iliyoko kwa raia kwamba wakimbizi wanapata kila kitu na sisi wenyewe hatupati chochote," mwisho wa kunukuu.
Kansela Merkel yeye amekuwa akisema kwamba anataka maelewano kuhusiana na serikali ya mseto yafikiwe kufikia katikati ya mwezi Januari.
Ujerumani imekuwa ikitaka nchi za EU zigawane wakimbizi
"Tutakuwa tunafanya mazungumzo hadi katikati ya mwezi Januari, huu ndio mpango uliopo. Na masuala ya Ulaya bila shaka yatakuwa katika ajenda na kulingana na sisi tutakuwa na mazungumzo ya serikali ya mseto muda mfupi baada ya hapo, kwa hiyo nafikiri hilo litawezekana iwapo mazungumzo na SPD yatafanikiwa," alisema Merkel.
Ujerumani imekuwa ikishinikiza bila mafanikio kwamba, nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya wagawane kwa usawa idadi ya wahamiaji kutoka Mashariki ya Kati na Afrika, huku nchi nyingi za Umoja huo kutoka Ulaya Mashariki zikipinga wazo hilo. Ila Gabriel anasema Umoja wa Ulaya unaweza kuanzisha mpango utakaozisaidia kwa pesa serikali za majimbo katika nchi maskini.
Merkel ambaye serikali mpya ya mseto kati ya Wahafidhina na SPD ndiyo nafasi yake nzuri ya kuwa Kansela kwa muhula wa nne amelalamikia wasiwasi kuhusiana na suala la uhamiaji kwa kule kupoteza kwake uchaguzi wa Septemba 24 na sasa anakubali kuchukuliwa msimamo mkali wa kurejeshwa makwao wahamiaji wanaokabiliwa na makosa ya uhalifu.
Mwandishi: Jacob Safari/Reuters
Mhariri: Gakuba Daniel