Misri, Eritrea na Somalia kushirikiana kiusalama
11 Oktoba 2024Mkutano huo wa kilele uliofanyika hapo jana katika mji mkuu wa Eritrea Asmara uliashiria kuanzishwa kwa muungano mpya wa kikanda katika eneo hilo la Pembe ya Afrika huku Ethiopia ambalo ni taifa la pili kwa idadi kubwa ya watu likiachwa nje ya mpango.
Uhusiano umezidi kuzorota kati ya Ethiopia na nchi jirani ya Somalia ambayo ilikasirishwa na mkataba wa bahari na Somaliland na tangu wakati huo imejiweka karibu na mpinzani wa muda mrefu wa Addis Ababa, Cairo.
Mkutano huo wa pande tatu mjini Asmara uliitishwa na Rais wa Eritrea Isaias Afwerki na kuwajumuisha wenzake wa Misri Abdel Fattah al-Sisi na Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.
Soma pia:Ethiopia ina wasiwasi juu ya Misri kupeleka silaha Somalia
Baada ya mazungumzo hayo ya nadra viongozi hao walitoa taarifa ya pamoja ambapo waliahidi kuimarisha uhusiano wa pande tatu katika nia ya kuboresha uthabiti wa kikanda. Bila kutaja taifa lolote walisema kunahitajika "heshima isiyo na shaka kwa mamlaka, uhuru na uadilifu wa eneo la nchi hizo."
Aidha, walisisitiza pia umuhimu wa "kukabiliana na uingiliwaji wa masuala yao ya ndani ya nchi za kikanda kwa kujiegemeza katika uhalali wa aina yoyote" na kuratibu juhudi za pamoja za kufikia lengo la utulivu wa eneo na kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya maendeleo endelevu ya pamoja.
Somalia imekuwa ajenda kubwa kwenye mkutano
Ama wakiangazia Somalia, viongozi hao kwa kauli moja wamekubaliana kulisaidia taifa hilo "kukabiliana na changamoto zake za ndani na nje na kuliwezesha Jeshi la Taifa la Somalia kukabiliana na ugaidi na kulinda mipaka yake ya nchi kavu na baharini.
Wasiwasi kuhusu uthabiti wa eneo hilo tete umeongezeka hasa kuhusu vita vinavyoendelea vya Sudan, mapatano yenye utata kati ya Ethiopia na eneo lililojitenga la Somalia la Somaliland na hata usalama katika bahari ya shamu ambapo waasi wa Houth wa Yemen wameendeleza mashambulizi yasiyo na kipimo kwenye vyombo vya majini.
Soma pia:Umoja wa Mataifa wawaomba wafadhili kuisaidia Somalia
Kama sehemu ya matokeo Somalia imesema mwishoni mwa mkutano huo kwamba, imepokea pendekezo la Misri la kupeleka wanajeshi nchini humo kama sehemu ya ujumbe wa kulinda amani wakati kikosi cha sasa cha Umoja wa Afrika kitakapomaliza muda wake mwezi Desemba.
Serikali ya Somalia imekuwa ikiinguwa mkono na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika tangu mwaka 2007 katika kupambana na kundi la itikadi kali la al-Qaida ambalo limekuwa likihusika na mashambulizi ya mara kwa mara katika taifa hilo.