1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Misri kuwa mwenyeji wa mkutano wa kutafuta amani Sudan

Sylvia Mwehozi
9 Julai 2023

Misri itaandaa mkutano wa kutafuta njia za kumaliza mapigano yaliyodumu kwa wiki 12 nchini Sudna baina ya makamanda hasimu wa kijeshi wakati Umoja wa Mataifa umekitoa tahadhari juu ya mzozo wa Sudan.

Abdul Fattah Al-Burhan na Mohamed Hamdan Dagalo
Majenerali hasimu wa Sudan kushoto ni Abdul Fattah Al-Burhan na kulia ni Mohamed Hamdan DagaloPicha: Bandar Algaloud/Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Misri itaandaa mkutano wa kutafuta njia za kumaliza mapigano yaliyodumu kwa wiki 12 nchini Sudan baina ya makamanda hasimu wa kijeshi. Taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais wa Misri imesema kuwa mkutano huo utakaofanyika Julai 13, unalenga kutengeneza mifumo madhubuti na mataifa jirani ili kupata ufumbuzi wa mzozo huo kwa amani kwa uratibu wa juhudi za kikanda na kimataifa. 

Wakati huohuo Umoja wa Mataifa umeonya kwamba, mzozo wa Sudanuko kwenye ukingo wa kutumbukia katika vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoweza kudhoofisha kanda nzima. Tahadhari hiyo imetolewa baada ya shambulio la anga katika makaazi ya raia lililosababishavifo vya watu 22.

Watu wapatao 3,000 wameuawa katika mzozo huo, huku manusura wakiripoti wimbi la ukatili wa kingono, mauaji ya kikabila na vitendo vikubwa vya uporaji.