Misri: Mamilioni wajimwaga mitaani
1 Februari 2011Ni wazi kuwa baada ya Jumanne ya leo (1 Februari 2011), Misri haitakuwa tena ile ya juzi na jana, iwe kwa kheri ama kwa shari.
Maandamano ya Watu Milioni Moja, kama waandaaji walivyoyaita, yataingia kwenye orodha ya matukio kadhaa ya kihistoria ya nchi hiyo kongwe na kubwa, nchi ya Musa na Haruna, ya Firauna na Hamana.
Bila ya kujali dini zao, Waislamu na Wakristo wa Misri wamekusanyika kumshinikiza Mubarak aondoke madarakani.
Kituo cha televisheni cha Al-Jazeera kimerusha picha ya umma kinaokisia kuwa ni zaidi ya watu milioni moja, wakipiga kelele, wakisali, wakiapiza na kulaani. Waandamanaji wamekuwa wakipaza sauti za: "Mungu ni Mkubwa!", "Mubarak ondoka!", na "Hatutaki Firauni mwengine!"
"Maisha yetu yote tumekandamizwa. Tuna hasira. Tunataka uhuru wa kuandamana. Uhuru wa kutoa maoni. Sasa sote tumeungana: Waislamu na Wakristo." Amesema muandamanaji mmoja wa kike.
Waandamanaji kuelekea Ikulu
Waandamanaji wanaripotiwa kuanza kujipanga, kuelekea kwenye makaazi ya Rais Mubarak yaliyo umbali wa kilomita 12 kutoka uwanja huo wa Tahrir.
Hata hivyo, inasemekana Mubarak mwenyewe hakai kwenye kasri hiyo tangu Jumanne iliyopita. Jeshi, ambalo limeahidi kutokutumia nguvu dhidi ya waandamanaji, tayari linaripotiwa kuzungusha seng'enge ya waya kwa kasri hiyo.
Wakati huo huo, upinzani umetangaza sharti la kuzungumza na serikali ni baada tu ya Mubarak kuondoka, kwa kile walichokiita kuwa Rais huyo tayari ameshapoteza uhalali wa kuitawala Misri, kwa mujibu wa mwanasiasa aliyeidhinishwa kuwakilisha matakwa ya upinzani, Mohammed El-Baradei, alipozungumza na kituo cha Televisheni cha Al-Arabiya.
"Kutakuwepo na majadiliano lakini ni baada ya matakwa ya umma kutimizwa, na la kwanza ni kuondoka kwa Rais Mubarak. Natarajia kuiona Misri ikiwa na amani, lakini huko kunategemeana na kuondoka kwa Mubarak. Akiondoka tu, kila jambo litakwenda vyema."
Mwanzo wa mwisho wa Mubarak
Mubarak, mwenye miaka 82, aliingia madarakani miaka 30 iliyopita, baada ya kuuawa kwa mtangulizi wake, Anwar Saadat. Akitokea kwenye ukamanda wa jeshi la anga, Mubarak alifanikiwa kupata uungwaji mkono wa mataifa ya Kimagharibi, ikiwemo Marekani, kwa siasa zake za maridhiano na Israel, lakini alifeli kwenye siasa za ndani kufuatia hatua zake utawala wake kukandamiza uhuru wa kisiasa.
Tukio la mwisho la kufeli kwa siasa zake za ndani, ni uchaguzi wa mwezi Novemba, mwaka jana, ambapo wizi wa kura na vitendo vya uvunjaji haki za binaadamu, ulimalizikia kwa chama chake cha NDP kupata kiasi ya asilimia 90 ya viti bungeni, lakini kikapoteza moja kwa moja imani ya wananchi, ambao walikuwa wanasubiri fursa tu ya kutolea hasira zao.
Maandamano ya umma yaliyomng'oa madarakani kiongozi mwenzake wa Kiarabu, aliyetawala kwa mfano wake, Zine al-Abidine Ben Ali wa Tunisia, hapo katikati ya mwezi uliopita, yanasemekana kuwa mfano uliowapa nguvu Wamisri kuchukua hatua kama hiyo.
Kwengineko ulimwenguni, wito wa kumtaka Mubarak akubaliane na matakwa ya umma umeendelea kutolewa, na safari hii ni kutoka kwa Waziri Mkuu wa Uturuki, Tayyib Erdogan, ambaye amenukuliwa na Shirika la Habari la Reuters, akimtaka Mubarak amuogope Mungu, na azuie damu ya ndugu zake wa Kimisri kumwagika. Erdogan amefuta ziara yake ya siku mbili iliyokuwa ifanyike nchini Misri wiki ijayo.
Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AFPE/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman