Misri, Sudan, Ethiopia zashindwa kuafikiana kuhusu bwawa
10 Januari 2020Misri, Sudan na Ethiopia zimeshindwa kufikia muafaka baada ya mazungumzo ya siku mbili juu ya mzozo kuhusu bwawa kubwa la umeme linalojengwa na Ethiopia kwenye mto Nile.
Hata hivyo Misri imesema inayo matumaini kuwa makubaliano yatapatikana kabla ya tarehe 15 Januari, ambayo ni muda wa mwisho waliokubaliana na Marekani.
Waziri wa maji wa Misri Mohammed Abdel Aty amewaambia waandishi wa habari mjini Addis Ababa, kwamba nchi hizo zimeweza angalau kukubaliana juu ya masuala muhimu, likiwemo lile la namna ya kulijaza maji bwawa hilo linalojengwa na Ethiopia.
Hata hivyo, mwenzake wa Ethiopia Sileshi Bekele, ameishutumu Misri kuja kwenye meza ya mazungumzo bila nia ya kufikia makubaliano.
Wajumbe wa nchi hizo tatu watakutana tena mjini Washington Januari 13, ambapo waziri wa fedha wa Marekani Steven Mnuchin na rais wa Benki ya Dunia Davis Malpass watashiriki.