Misri yachapwa bao 1-0 na Uruguay
15 Juni 2018Mchezo wa kwanza hii leo katika siku ya pili ya michuano ya kombe la dunia kati ya Misri na Uruguay umemalizika kwa ushindi wa Uruguay wa bao 1-0 lililowekwa wavuni katika dakika ya 89 ya mchezo kwa kichwa na Jose Gimenez katika mchezo wa kundi A.
Mshambuliaji wa Misri Mohamed Salah aliachwa nje ya uwanja licha ya kocha Hector Cuper kusema alikuwa katika hali nzuri kuweza kucheza katika mchezo huo kutokana na maumivu ya bega aliyopata katika mchezo wa fainali ya Champions League kati ya liverpool na Real Madrid mwezi uliopita.
Misri walipambana kiume lakini Uruguay walipata nafasi nzuri zaidi ambapo mshambuliaji wa Barcelona Luis Suarez alikosa nafasi nyingi za wazi na Edson Cavanni alipiga mpira uliogonga nguzo wa goli katika mpira wa adhabu. Mchezo mwingine unaoendelea hivi sasa ni kati ya Morocco dhidi ya Iran.
Usiku kutakuwa na pambano la kukata na shoka wakati mabingwa wa Ulaya Ureno watapambana na mabingwa wa zamani Uhispania.