1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yaomboleza vifo vya watu 41 kufuatia mkasa wa moto

15 Agosti 2022

Misri imefanya mazishi ya watu 41 waliopoteza maisha katika mkasa wa moto uliozuka ndani ya kanisa moja la wakristo wa madhehebu ya Coptic wakati wa ibada jana Jumapili.

Ägypten Giza | Feuer in Kirche
Picha: Mohamed Abd El Ghany/REUTERS

Mamia ya watu walijitokeza kutoa heshima za mwisho kwa miili ya wahanga wa mkasa mbaya kabisa wa moto uliogharimu maisha ya watu 41 na kujeruhiwa wengine 14.

Mkasa huo ambao mamlaka zimesema ulitokana na hitilafu ya umeme ulitokea kwenye kanisa la Abu Sifin lililopo katika wilaya yenye idadi kubwa ya watu ya Imbaba nje kidogo ya mji mkuu wa Misri, Cairo.

Kanisa hilo ni miongoni mwa mengi yanayotumiwa na waumini wa kikristo wa madehebu ya Coptic nchini Misri ambao idadi yao inafikia milioni 10. Ibada ya mazishi iliyofanyika kwenye viunga vya makanisa mawili ya Coptic katika mji mdogo uitwao Giza magharibi mwa mto Nile.

Vilio vilitanda pale majeneza yenye mabaki ya miili ya wahanga ilipofikishwa kanisani. Ndugu, jamaa pamoja na waumini wengine walijaribu kuyafikia majeneza na kuyashika huku wakibubujikwa machozi. Miongoni mwa waliopoteza maisha ni mchungaji wa kanisa lililotekekea kwa moto padri Abdel-Messih Bekhit.

Wahanga walipambana kunusuru maisha yao bila mafanikio 

Polisi wakishika doria kwenye viunga vya kanisa lililokumbwa na motoPicha: Mohamed Abd El Ghany/REUTERS

Moto ulizuka mnamo saa tatu asubuhi na kuzuia lango la kuingilia kanisani hali iliyofanya iwe vigumu kwa kiasi waumini 1,000 waliokuwemo ndani kutoka nje ya kanisa.

Walioshuhudia  mkasa huo wameeleza jinsi waumini walivyojirusha kupitia madirisha baada ya moto kutanda ndani ya jengo hilo lenye ghorofa kadhaa.

Saied Tawfiq, ni mmoja ya watu waliokuwepo eneo la tukio na amesema "baadhi ya watu walijitupa kupitia madirisha kujinusuru na moto. Ukitizama gari ya padri Abdul Masih utaona imebonyea kwa sababu mtu mmoja alijitupa kutoka dirishani kuepuka kifo, na sasa amelala hospitali anatibiwa majereha ya mkono na mgongo"

Mashuhuda wengine wamezungumzia namna watu waliokuwa nje, walivyoingia ndani ya jengo linalowaka moto kujaribu kuwaokoa waliokwama.

Inaaminika wengi walizidiwa na joto na moshi mzito na yumkini ndiyo sababu ya idadi kubwa ya vifo. Katika taarifa yake wizara ya mambo ya ndani ya Misri imesema uchunguzi umebaini moto ulianza kwenye kiyoyozi kimoja katika ghorofa ya pili kutokana na hitilafu ya umeme.

Wengi waghadhabishwa na kuchelewa kwa msaada wa uokozi 

Vikosi vya uokozi vimelaumiwa kwa kuchelewa kufika eneo la tukio Picha: Mohamed Salah/AP Photo/picture alliance

Hata hivyo wengi wanaulaumu jinsi vikosi vya uokozi vilivyoshindwa kufanya kazi haraka. Inaarifiwa magari ya kubeba yaliwasili karibu saa moja baada ya tukio na vivyo hivyo kwa magari ya kuzima moto ambayo kituo chake kipo umbali wa dakika tano tu kutoka lilipo kanisa.

Kufuatia mkasa huo rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi ametuma salamu za rambirambi kwa njia ya simu kwa Papa Tawadros II, ambaye ni mkuu wa kanisa la Coptic.

Kadhalika ameagiza mamlaka ya uhandisi ya jeshi kuchukua jukumu la kulijenga upya kanisa lililoteketea.

Salamu za rambirambi zimetolewa pia na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na viongozi wa taasisi kadhaa za kiislamu nchini Misri.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW