Misri yapeleka mzozo wake na Ethiopia baraza la Usalama
20 Juni 2020Misri inahofu kwamba bwawa hilo litapunguza kiasi cha maji inachohitaji kwa ajili ya shughuli muhimu katika nchi hiyo.
Hatua ya Misri inakuja siku chache baada ya duru ya mazungumzo kati ya Misri, Ethiopia na Sudan kuhusiana na bwawa hilo kumalizika bila ya kupatikana muafaka. Addis Ababa inatarajia kuanza kulijaza bwawa hilo la Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD) mwezi ujao.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Ethiopia imesema katika taarifa siku ya Jumamosi kuwa ombi la Misri linalitaka baraza la Usalama kuingilia kati ili kuhakikisha mazungumzo "kwa nia njema" baina ya nchi hizo tatu za mto Nile.
Misri "ilichukua hatua hii kutokana na kushindwa kwa mazungumzo ya hivi karibuni kuhusiana na bwawa hilo kutokana na msimamo hasi wa Ethiopia ambao unakuja katika mfumo wa kuchukua hatua katika msimamo ule ule katika muda wa muongo mmoja uliopita wa majadiliano hayo magumu," wizara hiyo imesema katika taarifa.
Lawaam kwa Ethiopia
Misri inailaumu Ethiopia kwa mkwamo huo , ikisema inakosa "nia njema ya kisiasa" kufikia makubaliano ya mwisho katika mzozo huo.
Ethiopia ilianza ujenzi wa bwawa hilo litakalozalisha umeme lenye thamani ya dola bilioni 4.8 mwaka 2010, kama sehemu ya mpango wa kupanua uuzaji wake wa nishati nje ya nchi.
Misri inategemea kwa kiasi kikubwa maji ya mto Nile kwa kilimo, viwanda na matumizi ya nyumbani ya maji na inahofia kuwa bwawa hilo litaathiri upatikanaji wa maji katika nchi hiyo. Ethiopia inasema hofu ya Misri haina msingi.