1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yasema Serikali ya Libya inashikiliwa mateka

16 Desemba 2019

Jenerali Khalifa Haftar ametangaza kuanzisha operesheni kubwa ya kufa na kupona kuudhibiti mji wa Tripoli na kuitimua serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa katika mji huo mkuu wa Libya

Libyen Premierminister Fayiz as-Sarradsch
Picha: picture-alliance/AP/P.D. Josek

Misri imesema serikali ya Libya inashikiliwa mateka mjini Tripoli na vikosi vya wanamgambo wenye silaha.Rais AbdelFatah El Sisi ametowa kauli hiyo jana Jumapili ikiwa ni siku chache baada ya jenerali muasi mwenye jeshi lake nchini Libya Khalifa Haftar kutangaza operesheni kubwa ya kuutwaa mji mkuu wa Tripoli ambako ndiko makuu makuu ya serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Kauli hii ya rais wa Misri ameitowa akiwa huko Sharm El Sheikh kulikofanyika mkutano siku ya Jumapili ambapo amesisitiza kwamba hali ya Libya inawatia mashaka na kwamba nchi yake ingeweza kuingilia kati nchini Libya lakini hawakuchukua uamuzi huo kwa kuheshimu hali ya nchi hiyo na kuuhifadhi mshikamano wa kidini. Lakini pia amesema usalama wa Misri umeathirika moja kwa moja kufuatia hali tete ya Libya.Juu ya yote al-Sisi amesisitiza kwamba kinachoendelea Libya ni kushikiliwa mateka kwa serikali kuu ya mjini Tripoli.

"Kile kinachoendelea Libya kwa kipindi cha miaka kadhaa na kwa nini serikali haina uhuru katika mji wa Tripoli ni kwa sababu inashikiliwa mateka na makundi ya wanamgambo yenye silaha pamoja na makundi ya kigaidi yaliyoko Tripoli.''

Jumapili hiyohiyo ubalozi wa Libya nchini Misri ulifungwa kwa muda usiojulikana sababu zilizotolewa zikiwa ni wasiwasi wa kiusalama. Taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa ubalozi huo imeeleza kwamba kufuatia sababu za kiusalama ubalozi huo utaendelea kufungwa kuanzia Jumapili bila ya kutolewa ufafanuzi zaidi.

Wanamgambo wanaoiunga mkono serikali ya TripoliPicha: AFP/M. Turkia

Lakini pia taarifa hiyo imekanusha ripoti nyingine zilizosambaa kwamba baadhi ya wafanyakazi wa ubalozi huo wamejitenga na serikali kuu inayotambulika iliyoko Tripoli.Hali hii inashuhudiwa wakati ambapo ndani ya Libya katika mji wa Tripoli kuna wasiwasi kufuatia tangazo la jenerali muasi Khalifa Haftar kwamba anaanzisha kampeini kubwa ya kijeshi ya kuutwaa mji huo wa Tripoli na kuitimua serikali kuu inayoungwa mkono Kimataifa. Haftar alitowa kitisho hicho siku nne zilizopita. Akizungumzia operesheni ya kuutwaa mji wa Tripoli Abdulla al- Thani  waziri mkuu wa serikali ya mpito iliyoko Mashariki mwa Libya mjini Tobruk ambayo inapingana na serikali ya Tripoli alisema.

''Tunamuomba Mungu ampe mafanikio mkuu wetu wa majeshi,jeshi na watu wote walioko kwenye eneo hili. Tunawaomba wananchi wetu katika mji wa Tripoli kusimama na jeshi kwasababu ndio njia pekee ya kupata uhai wa taifa hili na ushindi wa jeshi ndio utakaobadilisha kabisa mambo''

Picha: picture-alliance/AP Photo/Turkish Presidency

Miezi minane iliyopita Haftar alianzisha operehseni ya kuukamata mji wa Tripoli lakini wanamgambo wanaoshirikiana na serikali hiyo ya Tripoli walisaidia kuizuia operesheni hiyo ya Haftar ambayo haikufanikwa. Misri, Umoja wa falme za kiarabu na Saudi Arabia zinaonesha kusimama pamoja na Urusi katika kumuunga mkono Haftar wakati Qatar na Uturuki zinaaminika kuisadia serikali ya Tripoli.

Jumapili rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alifanya mazungumzo na waziri mkuu wa Libya Fayez al-Sarraj mjini Istanbul  ikiwa ni siku chache baada ya kiongozi huyo wa Uturuki kusema yuko tayari kupeleka wanajeshi Libya ikiwa ataombwa na Libya kufanya hivyo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Gakuba, Daniel

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW