1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yatangaza hali ya hatari baada ya milipuko kanisani

10 Aprili 2017

Rais wa Misri Abdel-Fatah al-Sisi ametangaza miezi mitatu ya hali ya hatari kufuatia mashambulizi mawili ya bomu ya kujitoa mhanga yaliyofanywa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu

Ägypten Alexandria Polizei Straßensperre
Picha: AFP/Getty Images

Milipuko hiyo iliwauwa watu 49 katika maadhimisho ya Jumapili ya Mitende, yakiwa ni mashambulizi mabaya zaidi kuwahi kufanywa dhidi ya wakristo walio wachache nchini humo katika siku za karibuni.

Mashambulizi hayo yaliyotokea katika miji ya jimbo la Nile Delta ya Tanta na Alexandria yalifuatia shambulizi la kanisa moja mjini Cairo mwezi Desemba na yalikuja wiki chache kabla ya ziara inayopangwa ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis inayonuia kuonyesha mshikamano na jamii ya Wakristo wa Misri walio wachache. Rais Sisi ametangaza ambayo lazima awasilishe bungeni ndani ya wiki moja. "Hatua kadhaa zitachukuliwa, kwanza ni kutangaza hali ya hatari baada ya kukamilika taratibu zinazofaa za kisheria na kikatiba kwa miezi mitatu nchini Misri. Tunatangaza hali hii ya hatari kwa kuilinda nchi yetu tu na kuzuia kuingiliwa kwa njia yoyote".

Watu 49 waliuawa katika milipuko miwili makanisaniPicha: Reuters/M. Abd El Ghany

Mlipuko wa kwanza katika kanisa la Mar Girgis mjini Tanta kaskazini mwa Cairo uliwauwa watu 27. Muda mfupi baadaye shambulizi jingine likatokea katika kanisa la Mtakatifu Mariko, mjini Alexandria ambako Kiongozi wa kanisa la Coptic Papa Tawadros wa pili alikuwa amekamilisha ibada ya Jumapili ya Mitende. Watu 17 wakiwemo polisi wanne waliuawa katika shambulizi hilo, ambalo wizara ya mambo ya ndani imesema lilisababishwa na mlipuaji wa kujitoa mhanga aliyejilipua wakati alizuiwa kuingia kanisani humo. Papa Francis ambaye anatarajiwa kuzuru Cairo Aprili 28 na 29, aliwaombea wahanga wa mashambulizi hayo. "Nnawaombea waliokufa na waliojeruhiwa. Mungu aibadilishe mioyo ya wale wanaoeneza ugaidi, machafuko na kusababisha vifo, na pia mioyo ya wale wanaotengeneza na kuingiza silaha".

Wapiganaji wa itikadi kali wanawatuhumu wakristo wa madhehebu ya Coptic kuwa waliliunga mkono mapinduzi ya kijeshi yaliyomwondoa madarakani rais Mohamed Morsi mwaka wa 2013, ambayo yalipelekea ukandamizaji mkubwa dhidi ya wafuasi wake. Desemba mwaka jana, mlipuko wa kujitoa mhanga uliodaiwa kufanywa na IS uliwauwa waumini 29 katika kanisa moja mjini Cairo.

Wacoptic ambao wataadhimishina Pasaka wikendi ijayo, wamekuwa wakilengwa na mashambulizi kadhaa katika miezi ya karibuni. Rais wa Marekani Donald Trump aliongoza kauli za kimataifa za kulaani mashambulizi hayo ya jana, akisema kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa ana imani kubwa kuwa Rais al-Sisi ataishughulikia hali hiyo ipasavyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea matumaini kuwa waliohusika na uovu huo watasakwa na kufikishwa mahakamani baada ya taarifa ya Baraza la Usalama kulaani milipuko hiyo ikiielezea kuwa ni ya "kinyama” na ya "uwoga”

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Caro Robi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW