1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yawapokea majeruhi kutoka Ukanda wa Gaza

Sylvia Mwehozi
1 Novemba 2023

Misri imepokea kundi la kwanza la raia wa Gaza waliojeruhiwa ambao wamefanikiwa kuvuka mpaka kupitia kivuko cha Rafah huku pia mamia ya raia walio na pasi za kusafiria za kigeni nao wakianza kuondoka eneo hilo.

Kivuko cha Rafah
Waandishi wa habari wakipiga picha za magari ya kubeba wagonjwa katika lango la kivuko cha RafahPicha: Mohammed Abed/AFP/Getty Images

Kundi la kwanza la watu waliojeruhiwa kwenye vita vya Israel dhidi ya Hamas, wameweza kuingia Misri leo kutoka Ukanda wa Gaza kupitia kivuko cha Rafah kufuatia makubaliano yaliyoratibiwa na Qatar. Majeruhi hao walipokelewa na timu ya maafisa wa afya ambao walikuwa wakiwaelekeza moja kwa moja hospitali, kulingana na vyanzo kutoka Misri.

Misri imeandaa kituo cha muda cha matibabu cha kuwapokea majeruhi katika mji wa Sheikh Zuweid uliopo kilometa takribani 15 kutoka Rafah na pia itawapeleka wagonjwa wengine kwenye hospitali nyinginezo za karibu.

Magari ya kubeba wagonjwa yapatayo 40 yameshuhudiwa yakiingia katika kivuko cha Rafah, huku umati mkubwa wa raia wa kigeni na wale wenye uraia pacha wakikusanyika karibu na kivuko hicho kwa matumaini ya kukimbia eneo hilo. Mpalestina huyo mwenye pia uraia wa Marekani kwa bahati mbaya hakuweza kuvuka hii leo.

"Mimi ni Mmarekani ninayeishi Gaza. Tulisikia kwamba kivuko kitafunguliwa, lakini kwa bahati mbaya tumegundua kuwa kwa sasa kimefunguliwa kwa mataifa maalum na ilitubidi tugeuze kwa sababu mtandao wa mawasiliano ulikuwa dhaifu na hatukujua kwamba kulikuwa na orodha. Tunatumai kuona majina yetu kwenye orodha ya kesho au siku inayofuata."

Wapalestina wakipekua eneo la makaazi lililoharibiwa na mashambulizi ya Israel katika kambi ya wakimbizi ya JabaliaPicha: Anas al-Shareef /REUTERS

Fuatilia habari hii: Guterres: Kuna hatari ya kutanuka mzozo wa Israel na Hamas

Chini ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya Misri, Israeli na Hamas, watu 81 waliojeruhiwa na orodha ya awali ya raia wa kigeni takribani 500 wataruhusiwa kuondoka Ukanda wa Gaza katika siku zijazo kulingana na duru tofauti. Hatua hiyo inakuja ikiwa ni zaidi ya wiki tatu tangu Israel ilipouzingira Ukanda wa Gaza na tangu wakati huo imeushambulia ukanda huo katika hatua ya ulipaji kisasi wa shambulizi la Hamas la Oktoba 7.

Soma kuhusu: Saudia yakosoa shambulio la Israel kambi ya wakimbizi Gaza

Wakati kukiwa na matumaini kwa baadhi ya raia kuyakimbia mapigano, kwa upande mwingine maelfu ya wananchi bado wamekwama ndani ya Gaza kwenyewe na kuendelea kukabiliwa na mashambulizi ya Israel ambayo hii leo yamelipiga jengo moja la makaazi katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia iliyoko Gaza City kwa siku ya pili mfululizo. Kwa mujibu wa serikali inayoongozwa na Hamas, mashambulizi hayo yamewaua watu wengi na wengine wamejeruhiwa.

Wizara ya afya ya Gaza inasema idadi ya vifo vya Wapalestina sasa imefikia 8,525 na katika Ukingo wa Magharibi zaidi ya raia 122 wameuawa katika machafuko yanayohusiana na uvamizi wa Israel. Hali ndani ya Gaza bado ni ya mashaka huku makundi ya misaada yakisema kuna upungufu wa chakula, mafuta na dawa kwa wakazi milioni 2.4.