1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misukosuko yazidi Venezuela baada ya uchaguzi

31 Julai 2017

Watu 10 wameuwawa nchini Venezuela wakati wa kupiga kura ya kulichagua bunge maalum la kuibadilisha katiba ya nchi hiyo. Marekani na nchi zingine kadhaa zasema hazitayatambaua matokeo ya uchaguzi huo.

Venezuela Caracas Nicolas Maduro
Picha: picture-alliance/dpa/M. Quintero

Tume ya uchaguzi nchini Venezuela imesema watu wapatao milioni nane ikiwa ni asilimia 41.53 wameshiriki katika zoezi la kupiga kura.  Raia hao wamepiga kura yenye utata ya kulichagua bunge maalum litakalo ibadilisha katiba ya nchi hiyo. Hata hivyo uchaguzi huo kwa kiwango kikubwa ulisusiwa na  baadhi ya  wananchi na uligubikwa na ghasia zilizosababisha mauaji. Kwa mujibu wa habari watu wasiopungua kumi waliuwawa katika mji mkuu wa Caracas na sehemu nyingine za nchi hiyo.

Vyama vya upinzani vinalalamika na kusema kuwa uchaguzi huo ulijawa na visa vya kuiba kura na kwamba kura hiyo ina lenga kumuongezea mamlaka rais Nicholas Maduro.  Kiongozi wa wapinzani Henrique Capriles ambaye pia ni gavana wa jimbo la kati la Miranda amesema harakati za upinzani zitafanyika leo katika mji mkuu wa Venezuela, Caracas ili pia kuwakumbuka watu walio uwawa wakati waliposhiriki kwenye maandano ya kuipinga serikali ya rais Maduro.

Machafuko ya VenezuelaPicha: Picture-Alliance/Zumapress/J. C. Hermandez

Waandalizi wa maandamano ya wapinzani wamesema watu 15 waliuwawa wakati wananchi walipokuwa wanapiga kura hapo jana.  Ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu imethibitisha kwenye mtandao wa Twitter kwamba inachunguza vifo visivyopungua saba. Wapinzani wanawalaumu viongozi wa serikali ya Venezuela kwa umwagikaji damu lakini

Waziri wa ulinzi wa Venezuela Jenerali Vladimir Padrino Lopez amesema jeshi la Venezuela halina lawama juu ya vifo vilivyotokea na ametowa mwito kwa ulimwengu uheshimu maamuzi ya raia wa nchi hiyo.  Rais wa Marekani Donald Trump amesema anatafakari kuiwekea Venezuela vikwazo katika sekta ya nishati.  Vikwazo hivyo vitaiathiri kampuni ya mafuta ya Venezuela (PDVSA) ambayo tayari ni dhaifu.

Mpaka sasa watu zaidi ya 120 wameshauwawa katika kipindi cha miezi minne iliyopita kutokana na mvutano baina ya wapinzani na serikali ya rais Nicholas Maduro. Rais Maduro amesema uchaguzi huo una lengo la kuutatua mgogoro wa kiuchumi na kisiasa nchini Venezuela, lakini wapinzani wa serikali wanasema kura hiyo itaua demokrasia katika taifa hilo la Kusini mwa Amerika. Marekani,Uingereza, Colombia, Mexico,Panama,Peru,Uhispania, Canada na mashirika kadhaa ya kimataifa yamesema hayatotambua matokeo ya kura hiyo.

 Rais Maduro aliitisha kura hiyo baada ya serikali yake kukumbwa na upinzani mkubwa hatua ambyao imeitumbukiza Venezuela katika mzozo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.

Mshirika muhimu wa Rais Maduro Diosdado Kabello amesema wananchi wengi walishiriki katika kupiga kura hapo jana na kwamba wapinzani  wanaodai kwamba ni watu wachache tu walioshiriki watashangaa.

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE/APE/AFPE

Mhariri:Iddi Ssessanga

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW