1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miujiza ya mawingu

28 Machi 2017

Mawingu ni muhimu katika mabadiliko ya hewa na joto duniani. Lakini wanasayansi wangali wanashangazwa jinsi mawingu yanavyobadilika kila siku na yanavyoibua changamoto katika utabiri wa hali ya anga.

Tequila Cloud im Urban Spree Berlin
Picha: DW/M. Sierra Alonso

Je unayaelewa mawingu? Japo tunayaona kila siku, mawingu husalia mwujiza. Kwa wanasayansi hali ya kutoeleweka kwa mawingu ni changamoto kubwa dhidi ya utabiri wa mabadiliko ya hali ya hewa. 

Mawingu huchukuliwa kama vitu vya kawaida katika maisha yetu. Lakini ni kati ya vitu ambavyo watu hawana ufahamu wa kutosha kuvihusu hasa kuhusiana na masuala ya mazingira. Hali inayowakunisha vichwa mno watafiti wanaojaribu kutabiri masuala yanayofungamana na mabadiliko ya tabia nchi.

Licha ya umuhimu wao kuhusu upatikanaji wa maji katika sayari ya dunia na jinsi joto linavyobadilikabadilika, wanasayansi wangali wanashangazwa na jinsi mawingu yanavyobadilika kila siku. Hawawezi kusema kwa uhakika jinsi mawingu yatakavyokuwa wakati wowote kufuatia ongezeko la joto katika mazingira. Hiyo inamaanisha kuwa hawawezi kufanya utabiri kamili wa jinsi dunia itakavyoathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Picha ya mawingu iliyonaswa na satelaitiPicha: picture-alliance/AP Photo/NOAA

Lakini sasa wanasayansi wanacho kifaa kipya cha kipimo ambacho ni 'atlasi' kwa lugha ya watabiri kufichua siri iliyoko. Atlasi ya kidijitali na ya kimataifa iliyozinduliwa na Shirika la Dunia la utabiri wa hali ya anga WMO. Atlasi hiyo ya kisasa iliyozinduliwa tarehe 23 mwezi Machi mwaka huu ni bora zaidi ya ile ya zamani ambayo imetumika tangu miaka 150 iliyopita.

Isabelle Ruedi ambaye ni afisa katika Shirika la WMO aliliambia shirika la habari la DW kuwa ''mara ya mwisho atlasi ya zamani ilitumiwa kupata vipimo ni takriban miaka 40 iliyopita. Wakati huo hakukuwa na internet, hakukuwa na kamera za kidijitali na mengine kama hayo. Inamaanisha kuwa siku hizi atlasi ya zamani haiwafikii watu wengi, hivyo tuliamua kuibadilisha tukizingatia elimu bora tuliyo nayo kuyahusu mawingu''.

Katibu mkuu wa shirika la WMO Petteri Taalas alisema atlasi hiyo inatoa nafasi kwa wataalamu wa anga na wanasayansi kuelewa kwa undani mawingu kwani hadi sasa bado hayaeleweki kikamilifu na wengi.

Katibu Mkuu wa WMO Petteri TaalasPicha: Reuters/D. Balibouse

Toleo hili jipya la atlasi kwa mara ya kwanza inaleta data au maelezo muhimu yakiwemo ya kiteknolojia ya hali ya juu kuhusu hali ya dunia na anga zake.

Mawingu ni muhimu katika mabadiliko ya hewa kwa kuwa yanahamisha maji kutoka sehemu moja au nyingine, mfano kuyapokea kutoka maziwa, mabwawa au mito na kuyapeleka katika nchi kavu kama mvua. Lakini mienendo yao inapopindukia, husababisha ukame na hata mafuriko. Mawingu pia hudhibiti viwango vya joto kwa kukinga miale ya jua. Kile tusichojua ni jinsi mienendo yao itakavyobadilika dunia inavyoendelea kuwa na joto.

Sandrine Bonny ambaye alichapisha ripoti ya utafiti wa sayansi ya hewa uliofanywa na shirika la utafiti duniani, anasema siri kuhusu mawingu zimeendelea kuhangaisha na ni ngumu kuzisuluhisha. Watafiti wanatumai kutumia maelezo mapya yatakayokusanywa na atlasi hiyo mpya kulenga mikakati ya kuzidisha elimu na ufahamu wa jinsi mienendo ya mawingu ilivyo kati ya miaka mitano na kumi ijayo.

Wataweka vipimo vipya kubaini mbona kumekuwa na mabadiliko mengi kuhusu majaribio yaliyofanywa kuhusu mienendo ya mawingu, uhusiano wa mawingu na kile kinachofanya maji kuyeyuka kuelekea angani na mabadiliko yanayofanyika sasa kutokana na ongezeko la joto.

Mwandishi: John Juma/ DW/

Mhariri:  Yusuf Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW