1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mivutano inazidi kushuhudiwa EAC

16 Januari 2024

Kuongezeka kwa mivutano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, kumewashtua wachambuzi wa mambo wakionyesha wasiwasi kuhusu hatma ya Jumuiya hiyo

Kenya Airways Flughafen Nairobi ARCHIV
Shirika la Ndege la Kenya Airways ni miongoni mwa yale makubwa kabisa barani AfrikaPicha: picture-alliance/dpa

Tanzania na Kenya zinarejea tena katika mivutano inayohusu sekta ya usafiri wa anga, ikilenga mashirika yake  lile Air Tanzania na Kenya Airways, mashirika ambayo yamewahi kutumbukizwa katika hali hiyo miaka ya nyuma.

Kuibuka tena kwa mvutano huo kunazusha maswali kuhusu namna mataifa hayo mawili yanavyoitazama sekta hiyo ya usafiri na kwamba hali hiyo inakuja wakati Tanzania ikianza kuimarisha tena usafiri wake wa anga baada ya kuongeza ndege ya mizigo.

Tayari  nchi hizo zimesema zinafanya juhudi kuutatua mvutano uliozuka baina yao baada ya Tanzania kutangaza kufuta kibali cha safari za ndege za abiria za shirika la Kenya Airways kati ya Nairobi na Dar es Salaam.

Kenya, Tanzania kutatua mvutano sekta ya usafiri wa anga

Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Tanzania, TCAA, ilitangaza mnamo Jumatatu jioni kufuta kibali hicho kwa ndege za shirika hilo la Kenya ikiwa ni kujibu msimamo wa serikali mjini Nairobi wa kukataa kutoa kibali cha kuingia Kenya kwa ndege za mizigo za kampuni ya ndege ya Tanzania, ATCL.

Baadhi ya wachambuzi wanaonya kuhusu kujirudia rudia tena kwa mazingira ya namna hiyo wakisema yanazuia utengamao mwema wa kiuchumi hasa wakati huu ambako sekta ya utalii ni kipaumbele kikubwa kwa Tanzania.

Mchambuzi Nicolas Clinton hata hivyo, anasema uzoefu wa pande hizo mbili kumaliza mivutano ya kiuchumi na kibiashara kwa njia ya mazungumzo ni ishara njema.

Baadhi ya nchi wanachama wa EAC bado wapo katika hali mbaya ya mahusiano

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zikiorodheshwa katika picha hii inayoonesha ramani ya nchi hizoPicha: Presidential Press Unit Uganda

Hayo yanajiri katika wakati ambapo baadhi ya nchi wanachama katika eneo hilo zikiingia katika uhasama mkubwa na kusababisha hali ya wasiwasi kuhusu hamta ya jumuiya yenyewe.

Rwanda kwa muda mrefu imekuwa ikikwaruzani na Jirani yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, huku  Kinshasha ikiinyoshea kidole Kigali kwa madai ya kujiingiza kijanja katika mizozo ya ndani kwa shabaha ya kuchota rasilimali zake.

Licha ya madai hayo kupuuziliwa mbali na utawala wa Rais Paul Kagame, ripoti za mashirika ya Umoja wa Mataifa bado zinaendelea kuitaja Rwanda kuwa ni moja ya kichocheo cha mizozo inayoendelkea kutokota nchini Kongo.

Wafanyabiashara Uganda walia na Burundi kufunga mpaka na Rwanda

Wakati mzozo huo ungali mbichi, mwanachama mwingine wa Afrika Mashariki Burundi imejitokeza na kuishutumu Rwanda kuwa ni sehemu ya wafadhili wa waasi wanaofanya mashambulizi Burundi.

Ikionyesha kukasilika kwake, hivi karibuni Burundi imetangaza kufunga mpaka wake na Rwanda, ikiwa wiki mbili baada ya kuituhumu nchini hiyo jirani yake kuunga mkono waasi wa kundi la RED-Tabara, waliofanya mashambulizi kwenye ardhi yake.

Mivutano inazidi kutokota ndani ya chombo hicho cha kikanda kilichoasisiwa na nchi wanachama watatu, Tanzania, Kenya na Uganda kabla ya kupanuka na kuzileta pamoja nchi za Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Jamhuiri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na hivi karibuni zaidi Somalia.

Mwandishi: George Njogopa, DW Dar es Salaam