1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Jumuiya ya kimataifa imesahau mizozo ya barani Afrika?

7 Juni 2024

Mashirika ya misaada yameonya juu ya mateso na ukosefu wa utulivu kunakosababishwa na kusahauliwa kwa mizozo na ufadhili mdogo kwa wakimbizi barani Afrika.

Mwanamume mzee akiwa na Punda wake wakipumzika huko Sudan.
Mwanamume mzee akiwa na Punda wake wakipumzika huko Sudan.Picha: AFP/Getty Images

Kulingana na ripoti ya kila mwaka ya Baraza la Wakimbizi la Norway NRC,  imeainisha mizozo 10 ya mwaka iliyopita iliyosahaulika na iliyochochewa kwa kiasi kikubwa kisiasa, kijamii na kifedha.

Baadhi ya mizozo hiyo ni ile iliyotokea katika mataifa ya Afrika Magharibi na kati au katika mataifa  jirani.

Mizozo ya nchi 10 iliyosahaulika ni pamoja na Burkina Faso, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mali, Niger, Honduras, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad na Sudan.

Mwezi Aprili shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR liliripoti uwepo wa zaidi ya wakimbizi na watu waliokosa makaazi milioni 12, katika maeneo ya Magharibi na Afrika ya kati.

Katika nchi Jirani ya Kongo na Sudan kunasemekana watu zaidi ya milioni 14 ni wakimbizi wa ndani huku maelfu ya wengine wakitafuta hifadhi katika mataifa jirani. 

Soma pia:Madaktari wasio na mipaka wasema watu 123 wafa kwa mapigano Sudan

Abdouraouf Gnon Kondé, ni mkurugenzi wa UNHCR upande wa Afrika Magharibi na Kati amesema watu wengi wanatafuta ulinzi karibu na mipaka ya nchi yao, lakini akatahadharisha kwamba hilo linaweza kubadilika iwapo hali itabadilika na kuwa mbaya zaidi pamoja na kutokuwa na usaidizi wa ndani.

Konde ameliambia shirika la habari la dpa kwamba watu wengi waliopoteza makazi ni wakulima na wafugaji ambao hawataki kuikimbia nchi yao.

Abdouraouf Gnon Kondé amesema   wasiwasi zaidi unaelekezwa kwa vijana hasa uwezo wao wa kufikia elimu.

Ameongeza kuwa iwapo vijana watakosa elimu kuna hatari ya wao kuendelea kuhama hata nje ya mipaka ya mataifa yao. 

Ufadhili kwenye mataifa yenye migogoro

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiwa kwenye mkutano unaohusu mzozo unaoendelea wa Sudan.Picha: Aurelien Morissard/EPA

Mwezi Aprili zaidi ya dola bilioni 2.1 za msaada kwa ajili ya Sudan zilichangishwa katika kongamano la kimataifa la wafadhili lililoandaliwa mjini Paris, Ufaransa.

Hatua hiyi ilichukuliwa baada ya vita vya mwaka mzima huko, ambavyo vimesababisha mamilioni ya wakazi wake kuyakimbia makazi yao pamoja na matatizo mengine ya kibinadamu kama elimu, afya na baa la njaa. 

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, alisema lengo kuu la fedha hizo ni kuwasaidia watu milioni 51 wa Sudan na msaada huo unalenga kusaidia mahitaji muhimu ya kibinadamu ikiwemo chakula, maji, dawa na mahitaji mengine ya dharura na kusisitiza kwamba mgogoro wa Sudan kama migogoro mengine barani Afrika haijasahaulika katika ramani ya dunia. 

Soma pia:Watu 85 wauwawa kufuatia mapigano makali Sudan

Kando na Afrika mwezi uliopita, Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalowashuhgulikia wakimbizi, Filippo Grandi, alitahadharisha kwa ujumla kwamba idadi ya watu wanaoyakimbia makaazi yao kwa  sababu  ya  vita na vurumai duniani imefikia watu milioni 114 na idadi yao inaongezeka kwa sababu dunia imeshindwa kutatua vyanzo vya migogoro.

Grandi, alilikosoa  Baraza la Usalama lenye wajibu wa kulinda amani ya  dunia, kwa kushindwa kutumia uzito wake ili kuitatua migogoro ya Gaza, Sudan, Ukraine, Myanmar, Kongo  na kwingineko duniani. 

Grandi pia alizilaumu baadhi ya nchi kwa kupitisha maamuzi ya muda mfupi katika msingi wa undumakuwili.

Mkuu huyo wa shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR alisema nchi zinashindwa kutumia uwezo wao ili kuhakikisha utekelezaji wa sheria za kimataifa na hali hiyo inajenga mazoea miongoni mwa makundi fulani kuendeleza migogoro.

Vurugu zauwa watu 38 El-Fashir Sudan

01:16

This browser does not support the video element.



 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW