1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjadala kuhusu sheria ya uchaguzi Tanzania bado wafukuta

Deo Kaji Makomba
30 Januari 2024

Baadhi ya wadau wa masuala ya demokrasia nchini Tanzania wamendelea kuonyesha wasiwasi kuhusiana na maoni yaliyotolewa na wadau mbalimbali, kuwa huenda yasizingatiwe katika miswaada mitatu ya sheria na uchaguzi

Dodoma, Tanzania |  Dr. Tulia Ackson
Spika wa Bunge la Tanzania Dr. Tulia AcksonPicha: Ericky Boniphace

Hofu ya wadau hao inatokana na bunge la Tanzania kuwa la chama kimoja na hivyo wadau wa masuala ya demokrasia nchini humo wameonyesha wasiwasi wao endapo kama maoni ya msingi yaliyowasilishwa mbele ya kamati ya kudumu ya bunge, utawala, Katiba na sheria kama yatazingatiwa. 

Akizungumza na DW, mbunge wa zamani waCHADEMA John Heche anasema kuwa miswada mitatu iliyowasilishwa bungeni ni kama kiini macho na kwamba haijazingatia maoni ya wananchi na ni muendelezo wa Chama cha mapinduzi CCM, kuteka nyara uchaguzi ambao unawafanya wananchi waheshimike.

 Soma pia:Chadema: Maandamano yatafanyika kama yalivyopagwa

Miongoni mwa maoni yaliyowasilishwa na wadau wa demokrasia nchini Tanzania, ni pamoja na kutaka wakurugenzi wa halimashauri kutokusimamia uchaguzi na kiwepo  kifungu kitakachotoa takwa la ushindi wa uraiskuwa zaidi ya asilimia 50, ikiwa ni pamoja na matokeo kupingwa mahakamani, vyama vya siasa vyote kupewa ruzuku na uchaguzi wa serikali za mitaa usimamiwe na Tume ya Taifa ya uchaguzi NEC na si TAMISEMI.

Mapendekezo ya upinzani katika miswada

Hata hivyo Chadema ambacho ni miongoni mwa vyama 13 vya siasa vilivyowasilisha maoni yao kwenye kamati hiyo, kilipendekeza kufutwa na kuondolewa bungeni kwa miswaada ya sheria hizo na badala yake muswaada wa marekebisho ya katiba upelekwe bungeni.
 Soma pia:Tanzania yaahidi kuifanyia kazi sheria ya uchaguzi

Chadema waandamana kupinga mageuzi ya sheria ya uchaguzi

02:48

This browser does not support the video element.

Mdau wa masuala ya demokrasia na mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka katika kituo cha haki za binadamu nchini Tanzania, LHRC, wakili Maduhu William anasema kuwa kuna wasiwasi mkubwa endapo kama maoni yaliyotolewa na wadau yatazingatiwa.

Tayari ya kamati ya kudumu ya bunge, utawala, Katiba na sheria imewasilisha miswaada hiyo katika vikao vya bunge vilivyoanza Jumanne hii, kwa ajili ya kuijadili na kuchambua miswaada hiyo mitatu ya sheria na uchaguzi nchini Tanzania.