1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjadala mzito Bungeni Tanzania kufuatia kauli ya Gwajima

Deo Kaji Makomba
27 Mei 2025

Kauli ya mbunge wa chama tawala CCM, Josephat Gwajima, kuhusu masuala ya utekaji nchini Tanzania na kisha kutoa ushauri wake nini kifanyike ili kuondoa matukio hayo ya kikatili, imeibua mjadala katika Bunge la Tanzania.

Baadhi ya wabunge Tanzania wamshambulia Askofu Gwajima kwa kauli yake na kutaka afukuzwe uwanachama
Baadhi ya wabunge Tanzania wamshambulia Askofu Gwajima kwa kauli yake na kutaka afukuzwe uwanachamaPicha: DW/S. Khamis

Miongoni mwa viongozi wa dini waliotoka hadharani kumkingia kifua Askofu Gwajima, ni Askofu Emausi Mwamakula wa kanisa la uamusho la Morovian, ambaye amesema kuwa alichozungumza Gwajima sio kipya isipokuwa ni yale malalamiko ambayo viongozi wa dini, wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu na wanasiasa nchini Tanzania wamekuwa wakisema, isipokuwa watawala wanafumba macho.

Askofu Mwamakula ameenda mbali zaidi kwa kusema kuwa alichozungumza Gwajima ni kweli na ni hoja kubwa ambayo inapaswa kujibiwa kwa hoja na kwamba ipo haja ya kubadilisha mfumo wa utawala ikiwemo vyombo ulinzi na usalama viwe huru na utawala.

"Hivi vyombo vya usalama vinatumika, vinatumwa na mwenyekiti wa CCM, kwa hiyo aliyosema Gwajima ni yaleyale kwamba mwenyekiti wa CCM anamamlaka na vyombo hivyo. Nimesikiliza mjadala bungeni, hawa watu wanajipendekeza kwa mtawala, lakini bahati mbaya sasa hivi Watanzania wote wanajua kinachoendelea", alisema Mwamakula.

"Hivi tukae tuwe na mtu kama huyu ambaye anatusumbua..."

Kauli ya Askofu Josephat Gwajima kuhusu masuala ya utekaji nchini Tanzania yaibua mjadala mkali bungeniPicha: DW/S. Khamis

Kauli ya Askofu Gwajima imeibua mjadala katika bunge la Tanzania huku baadhi ya wabunge wakimshambulia Gwajima ambaye ni mbunge wa jimbo la Kawe kupitia CCM kuwa kauli aliyoitoa hivi karibuni inapaswa kulaaniwa. Abass Tarimba ni mbunge wa Kinondoni. 

"Kuna mtu mmoja humu ndani mwenzetu, mbunge, tena ana nafasi ya kuzungumza humu ndani, ana nafasi ya kuzungumza kwenye NEC, ana nafasi ya kukutana na wakubwa.. anaanza kutuchokonoa. Mimi nakiuliza chama changu CCM, huyu bwana ana kadi ya chama.. hivi tukae tuwe na mtu kama huyu ambaye anatusumbua...", alihoji Tarimba.

Jumamosi iliyopita, Askofu Gwajima alitoka tahadhari mbele ya waandishi habari jijini Dar es Salaam akilaani na kushutumu mambo yanayoendelea ya utekaji nchini Tanzania huku akisema kuwa kufuatia hali ilivyo hivi sasa nchini humu umefika wakati wa yeye kuongea na kukemea, kwani vinaathiri kwa kiasi kikubwa taswira ya taifa kimataifa na kuvuruga uhusiano wa kidiplomasia.

"Ninaomba niwaambie ukweli kwamba utekaji si utamaduni wa kitanzania, na ni jambo ambalo halitakiwi kuungwa mkono na mtu yeyote."

Askofu Gwajima alisema kuwa lengo ni kuyasema matukio hayo na kutoa ushauri na ufumbuzi wa matukio hayo ya utekaji.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW