Mjamzito mmoja hufa kila dakika mbili duniani - WHO
23 Februari 2023Ripoti iliyochapishwa siku ya Alhamis (23 Februari) na shirika hilo mjini Geneva ilisema, hata hivyo, idadi hiyo ya vifo ni ya chini kuliko hali ilivyokuwa miaka 20 iliyopita, ambapo vifo vya wanawake wajawazito ilikuwa 446,000 kwa mwaka, lakini ni ongezeko kubwa baada ya kushuka baina ya mwaka 2000 na 2015.
Kwa ujumla, idadi ya wajawazito wanaopoteza maisha imeshuka kwa asilimia 34.3 ndani ya miongo miwili iliyopita kutoka vifo 339 kwa kila wajawazito 100,000 mwaka 2000 hadi vifo 223 mwaka 2020, kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotayarishwa na WHO na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa.
Belarus ndiyo iliyosajili kupungua sana kwa vifo vya wajazito kwa tarkribani asilimia 96, huku Venezuela ikiwa na ongezeko kubwa kabisa. Baina ya mwaka 2000 na 2015, nchi iliyokuwa na ongezeko kubwa zaidi la vifo vya wajawazito ilikuwa Marekani.
Hali mbaya zaidi kusini mwa Afrika
Takwimu za WHO zinaonesha kuwa hali ni mbaya zaidi kwenye maeneo masikini na nchi zenye migogoro, ambapo mataifa ya Afrika yaliyo chini ya Jangwa la Sahara yalikuwa na asilimia 70 ya vifo kwa mwaka 2020, yakifuatiwa na ya Asia ya Kati na Kusini ambayo yalikuwa na asilimia 17.
Akiandika kwenye dibaji ya ripoti hiyo, Mkurugenzi wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisema kwamba "takribani kila kifo kinatokea kwenye nchi za vipato vya chini na kati, na takribani kila kifo katika hivyo kinaepukika."
"Hakuna mama yoyote anayepaswa kuhofia kupoteza maisha wakati wa kumleta mtoto hapa ulimwenguni, hasa katika wakati ambapo maarifa na vifaa vya kutibu matatizo yanayofahamika vipo. Uwepo wa usawa kwenye huduma za afya unampa kila mama, vyovyote alivyo na popote alipo, fursa sawa ya kujifungua salama na mustakabali mwema na familia yake." Alisema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, Catherine Russell.
Sababu zinazoepukika
Sababu zinazoepukika ambazo zinaweza kupelekea kifo zinajumuisha na kutoka damu sana, shinikizo la moyo, utoaji mimba usio salama na maradhi kama vile virusi vya Ukimwi na malaria.
Miongoni mwa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ni kupunguza vifo vya wajawazito kutoka 339 kwa kila wanawake 100,000 wanaojifungua mwaka 2000 hadi chini ya 70 ifikapo mwaka 2030. Katika mwaka 2020, idadi hiyo ilikuwa ni 223.
Kuongeza huduma ya uzazi salama na kuimarisha uwezo wa wanawake kujiamulia wenyewe kwenye masuala ya uzazi ni miongoni mwa hatua zinazopaswa kuchukuliwa kufikia lengo hilo, inasema ripoti hiyo.